KABUL, AFGHANISTAN

WAPIGANAJI wenye silaha kutoka kundi Taliban lililochukua mamlaka nchini Afghanistan, limewatawanya kwa nguvu kundi la wanawake ambao walikuwa wakitaka wasichana nchini Afghanistan kuruhusiwa kurejea skuli za sekondari kuendelea na masomo.

Maandamano hayo yalifanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Kabul, ambapo takribani wapiganaji 10 wa Taliban waliwahi katika eneo la tukio na kuwatishia wanawake kuondoka mara moja katika eneo hilo.

Wapiganaji hao waliokuwa na silaha walifuatua risasi hewani ikiwa ni tahadhari ya kuwataka wanawake hao wanaopanga maandamano kuondoka katika eneo hilo.

Wasichana nchini Afghanistan wanashindwa kuhudhuria skuli za sekondari kuendelea na masomo yao tangu kundi la Taliban ilipochukua udhibiti wa nchi hiyo mnamo katikati ya mwezi Agosti mwaka huu.

Mnamo mwezi Septemba mwaka huu, kundi hilo lilisema wavulana na wasichana katika skuli za sekondari hawawezi kusoma katika jengo moja ama darasa moja chini ya tafsiri ya mafundisho ya dini ya kiislam.

Hali ya wasiwasi juu ya kufunguliwa tena kwa skuli za sekondari kwa ajili ya wasichana inazidi kuongeza wasiwasi kuhusiana na makatazo zaidi ya haki za wanawake chini ya utawala wa Taliban.