SIKU chache zilizopita Zanzibar iliungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku adhimu ya wazee.
Uzee ni hatua ya mwisho katika hatua tatu kubwa za makuzi ambazo mwanadamu anayejaaliwa kupata umri mkubwa hupitia kabla ya kumalizika kwa maisha yake hapa duniani, ambapo kwa sababu ni hatua ya mwisho mara nyingi kuifikia huwa ni majaaliwa.
Hatua ya kwanza kabisa ya makuzi ya binaadamu hupitia kwenye utoto, ambapo kwa kawaida binadamu wa namna hii huwa tegemezi wa familia na hatua ya pili ujana ambapo katika hatua hii binaadamu huwa mwenye nguvu.
Unapomalizika ujana unaingia kwenye hatua ya mwisho ya uzee, ambapo wakati mwengine binaadamu hurejea kuwa tegemezi kama mtoto au hata zaidi ya mtoto, hata maandishi yanaeleza kuwa wakati wa uzee binadamu anaweza kuwa chini kuliko waliochini.
Katika hatua ya uzee binaadamu hukabiliwa na changamoto nyingi, lakini wakati mwengine hutegemea sana vipi alijipanga kukabiliana na hatua hiyo ya tatu akiwa wakati wa ujana na namna gani sera zilizopo nchini zinaweza kusaidia maisha ya wazee.
Ni katika kipindi cha uzee, ambapo mwanadamu huishiwa nguvu kutokana na seli za mwili kuzeeka, kuchoka na kupungukiwa na kinga ya mwili hali ambayo hukaribisha changamoto nyingi za kiafya.
Pamoja na umasikini, serikali ya Mapinduzi tangu awamu ya kwanza chini ya hayati mzee Abeid Amani Karume na awamu zote zilizofuata hadi kufikia awamu ya nane, imekuwa na sera bora katika kuhakikisha inastawisha maisha ya wazee.
Kwa kutambua umuhimu wa wazee hasa wale wasio na matunzo na waliokosa jamaa, serikali iliwajengea makaazi maalum Unguja na Pemba sambamba na kuwapatia huduma muhimu kama vile chakula, mavazi, pesa za kujikimu, huduma za afya nakadhalika.
Aidha katika kukabiliana na hali ya maisha serikali ikafikia uamuzi wa kuwapatia wazee waliofikia umri wa miaka 70 fedha maalum pencheni jamii ya shilingi 20,000 ambapo pamoja na kuwepo mawazo ya kuongezwa kiwango hicho, lakini bora kupata.
Ni muhimu tukafahamu kuwa pamoja na serikali kuimarisha sera nzuri za kusaidia ustawi wa wazee, lakini familia haziwezi kulikwepa jukumu la msingi la kuwalea, kuwapa matunzo, kuwapa upendo na kuwapa haki zao wazee kama binadamu wengine.