NA MWAJUMA JUMA

KINGA ni bora kuliko tiba, huu ni msemo wa kale uliotumiwa na wazee wetuambapo unahimiza umuhimu wa kutambua afya kama ndio msingi bora katika kujenga maisha bora ya kila siku.

Katika siku za hivi serikali imo katika kampeni kubwa za kuhamasisha watu kuchanja chanjo ya ugonjwa wa corona ambayo, pamoja na kuwa sio lazima lakini tuchukuwe tahadhari ya kuchanja ili kujikinga.

Tayari baadhi ya viongozi wetu wakuu wamejitokeza kuchanja ambapo na sisi kama jamii tunapaswa kuungana na viongozi wetu kupata chanjo hizo.

Pia jamii inatakiwa kuchukuwa tahadhari za kujikinga na maambukizi hayo ikiwemo kufuata ushauri wa kitaalamu, licha ya juhudi za watu kujitokeza kupatiwa chanjo.

Suala la kuchanja chanjo ya ugonjwa huo ni la hiari lakini ni jambo jema ambalo linapaswa kupewa umuhimu na wananchi na ni vyema wachukue hatua ya kuchanja katika kusaida kujenga kinga ya miili ili kupambana na maradhi hayo.

Kumekuwa na maneno mengi juu ya chanjo lakini ni vizuri jamii ikayapuuza maneno hayo na badala yake wafuate maelekezo na ushauri ambao unatolewa na wataalamu wa afya.

Jamii inapaswa kutambuwa kwamba pamoja na kuchanja pia ni vyema kuendelea kuchukua hatua za tahadhari za kujikinga na maradhi hayo kwa kuwa kuchanja pekee haizuii uwezekano wa kupata maambukizi ila inapunguza athari ya ugonjwa unapotokea.

Chanjo hiyo kwa maneno ya wataalamu wa afya inasaidia kujenga kinga ya mwili.Hivyo wananchi wanatakiwa kufahamu kwamba ni vyema pia kutambua mfumo na mwenendo wa dunia unavyokwenda hivi sasa kwa kuwa nchi nyingi duniani hawaruhusu kuingia nchini kwao bila ya kupata chanjo ya ugonjwa huo.

Tutambuwe kwamba chanjo za ugonjwa huo zinazotolewa ni salama na kwamba ni vyema wananchi wote kujitokeza kushiriki katika kujenga kinga ya mwili dhidi ya maradhi ya UVIKO 19.

Tunatambua kwamba kuna changamoto mbali mbali katika zoezi hilo lakini lichukuliwe ni moja ya fursa katika kuhakikisha zinatatuka.