NA SHAIBU KIFAYA, PEMBA

WAZAZI na Walezi wa Shehia ya Wawi Pemba, wametakiwa, kushirikana na
Waalimu wa Skuli ya Dokta, Omar Ali Juma, Sekondari na msingi katika
kufuatilia mienendo ya watoto wao wanapokuwa majumbani na hata wakati
wanapokuwa Skuli, ili kijikinga na matendo ya udhalilishaji na
ukatili wa kijinsia ambao unaweza kutokea dhidi yao.

Hayo yalielezwa na Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Chake Chake Pemba
Salma Khamis  Haji, huko katika Skuli hiyo  wakati  akizungumza na Waalimu, Wazazi na Kamati inayosimamia matendo ya udhalilishaji katika maeneo yao.

Alisema Serikali imeamuwa kuandaa mpango mkakati wa kutembelea  Skuli
mbali mbali kwa kutoa elimu ya kujikinga na matendo ya udhalilishaji
na ukatili wa kijinsia kwenye makundi tofauti ndani ya jamii, ili
kuweza kujikinga na matendo hayo.

“Ni wajibu wetu sasa sisi wadau tulio na dhamana ya kupita kila Skuli
ili kutowa elimu hii ya kujikinga dhidi ya matendo haya maovu ya
udhalilishaji na ukatili wa kijinsia, hasa kwa wanafunzi wa maskulini
kwani wao ndio waathirika wakubwa wanaokumbwa na vitendo hivi” alisema
Ofisa huyo.

Nae Ofisa Elimu Wilaya ya Chake Chake Pemba, Burhani Khamis  Juma,
alisema, ipo haja kwa Waalimu kuzudisha ulinzi Skulini hapo, ili kuwepo
kwa mazingira salama kwa wanafunzi, ili wapate kuepukana na matendo ya
udhalilishaji na ukatili wa kijinsia.

Kaimu Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo,  Said Ali Makame,
alisema wamekuwa wakifuatilia mienendo ya wanafunzi Skuli hapo, kwani
lengo ni kuondoa matendo yote ambayo hayaendani na maadili na nidhamu
katika jamii.

” Tumepanga kutoa adhabu kwa kila mwanafunzi yoyote atayebainika
kujihusisha kuwafanyia wanafunzi wenzake  vitendo hivyo na kuwa na
mwenendo usio mzuri  Skulini hapa ili kukomesha matendo hayo na hapo
baadae matarajio yetu ni kuondoka kabisa,” alifafanuwa Ofisa huyo.