NA ASYA HASSAN

MAOFISA kutoka ngazi mbalimbali za serikali na binafsi wametakiwa kutumia mbinu na busara pale wanapobaini kunaviashiria vyovyote vinavyosababisha uvunjifu wa Amani.

Wito huo ulitolewa na Claudia Maffettone kutoka Shirika la ‘Search for Common Ground’ alipokuwa akiwapatia mbinu na njia za utatuzi wa migogoro maofisa kutoka ngazi mbalimbali za serikali na binafsi kupitia mradi wake wa dumisha Amani Zanzibar.

Alisema maofisa hao wanafanya kazi karibu na jamii hivyo wamekuwa wakishuhudia changamoto mbalimbali, hivyo ni vyema wakatumia mbinu na busara katika kuondosha matatizo hayo hatimae jamii iweze kuishi kwa Amani.

Sambamba na hayo, alisema jamii imekuwa na mitazamo tofauti, hivyo ni vyema wanapokutana na tatizo hilo wakatumia hekma na busara, ili kusaidia kuiunganisha na kuondosha sitofahamu baina yao.

“Ni vyema munapokuwa katika hali hiyo basi musivamie wala kukurupuka kwanza muhimu kulitambue tatizo hatua hiyo itasaidia kuweza kutoa suluhi iliyokuwa sahihi,”alisema.

Alifahamisha kwamba wanapokutana na matatizo kunahitajika utaalamu na mbinu, ili kuifanya jamii hiyo iweze kukufahamu na kukuelewa na sio kushughulikia migogoro hiyo kimazoea.

Aidha, alifahamisha kwamba taasisi hizo zina zima na majukumu mapana katika kuisimamia jamii hivyo ni vyema wakaendeleza ushirikiano wao katika utekelezaji wa majukumu yao hatua ambayo itasaidia kuleta maslahi mapana katika kuwatumikia wananchi.

Baadhi ya washiriki wa Mafunzo hayo, walisema taaluma hiyo waliyopatiwa itawasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi.

Walifahamisha kwamba wao wamekuwa wakifanya kazi na jamii na kukutana na matatizo tofauti hivyo kupitia Mafunzo hayo itakuwa chachu ya kutatua migogoro mbalimbali inayojitokeza wakati wa kutekeleza majukumu yao.