NA HAFSA GOLO

WABUNGE  wa Chama cha Mapinduzi (CCM) majimbo ya mkoa wa Kaskazini ‘A’ Unguja, wameahidi kutumia fedha za mfuko wa jimbo katika bajeti ya fedha ya  2021 /2022 kwa kutatua changamoto mbali mbali,  ikiwemo ujenzi wa hospitali, barabara za ndani na mradi wa maji safi na salama.

Wakizungumza mbele ya  Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Job Ndugai,  hivi karibuni wakati alipofanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo  Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Walisema ujenzi wa miradi hiyo ni utekelezaji wa ahadi, uondoshaji kero za wananchi, pamoja na uimarishaji wa upatikanaji wa huduma za kijamii na kuleta mageuzi ya maendeleo majimboni.

Mbunge wa jimbo la Matemwe Yahya Ali Khamis, alisema  anatarajia kutumia shilingi  milioni 50  katika ujenzi wa mradi wa maji safi na salama  ili kuondosha kadhia ya muda mrefu  inayowakabili  wananchi wa Kigomani.

Alisema wananchi hao  zaidi ya miaka 10  wamekuwa wakitumia maji yakunywa  ya chumvi jambo ambalo limekuwa lililalamikiwa na wananchi hao .

“Niliahidi wakati wa kampeni tatizo hilo mara baada ya kunichagua nitalimaliza hivyo hivi sasa natekeleza ahadi hiyo ”,alisema.

Nae Mbunge wa Jimbo la Donge Dk.Soud Mohamed alisema  fedha za mfuko wa jimbo zote zitatumika kumaliza ujenzi wa hospitali jimboni humo ili kuimarisha  mahitaji ya upatikanaji wa huduma za afya ikiwemo upasuaji.

“Mimi na mwakilishi wakati tukipeperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi kuwanaia nafasi tuliahidi kwa pamoja kumaliza kilio cha wananchi cha ujenzi wa hospitali ya kisasa yenye kutoa huduma zote muhimu ikiwemo upasuaji,mama na mtoto na huduma nyengine”,alisema.

Suod alisema ili kuhakikisha mradi huo unakamilika  wataunganisha nguvu za pamoja  za jimbo hilo sambamba na kutafuta  wahisani wengine ili kuona hospitali hiyo inakamilika huku ikiwa na vifaa vyote vinavyohitajika katika utoaji wa huduma .

Mbunge wa jimbo la Bumbwini, Mbaruok Juma Khatib alisema, katika kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama sambamba na kumaliza kilio cha wananchi atatekeleza mradi wa maji safi na salama katika vijiji vinne jimboni humo.

Alibainisha vijiji hivyo ni Mangapwani, Fujoni, Zingwezingwe na Bubwini ambapo  alisema utekelezaji wa mradi huo  utatumika fedha za mfuko wa jimbo  shilingi milioni 14 .8.

Aidha mbunge wa jimbo la Tumbatu Juma Othman Hija , kuhusu fedha za mfuko wa jimbo, amekusudia kutumia kwa ajili ya kutilia mkazo suala la kilimo cha   biashara ya mboga mboga  kwa wajasiriamali wadogowadogo ili kupanua fursa za ajira.