NA MADINA ISSA
MKUU wa Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid amesisitiza umuhimu wa walimu kuendeleza michezo kwa wanafunzi maskulini.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu huyo, mkuu wa wilaya ya Kusini Unguja Rashid Makame Shamsi, katika hafla fupi ya kupokea makombe ya ushindi kwa wanafunzi walioshinda sherehe za elimu bila malipo zilizofanyika Pemba hivi karibuni.
Alisema suala la michezo kwa wanafunzi ni muhimu kwani mbali ya kujengeka kiafya na kiakili, lakini kunawaepusha na kujiingiza katika vitendo viovu ikiwemo utumiaji wa dawa za kulevya.
Aidha aliwapongeza wanafunzi hao kwa ushindi walioupata wa kuchukua nafasi ya tatu kati ya mikoa mitano ya Zanzibar hali iliyopelekea kuletea sifa mkoa huo.
Sambamba na hayo, aliwasihi kusoma kwa bidii ili kuweza kufanya vizuri katika masomo yao.
Kwa upande wake mratibu wa michezo wilaya ya Kati, Abdulwahad Dau Haji, aliwaomba wazazi na walezi kutoa mashirikiano kwa watoto wao, juu ya kushiriki michezo maskuli na kuondokana na dhana ya kwamba michezo inapelekea kufeli mitihani yao.
Nao wanafunzi walioshiriki michezo hiyo, wamesema mbali ya kupata ushindi lakini pia wamejenga uhusiano na wanafunzi kutoka skuli mbali mbali na kuwataka wanafunzi wenzao kutovificha vipaji vyao kwani michezo itaweza kuwapatia ajira.
Wanafunzi hao wamefanikiwa kupata makombe saba na medali 33 zikiwemo dhahabu 14, fedha 11 na shaba nane, zilizohusisha michezo tofauti ikiwemo mpira wa pete, mpira wa miguu, riadha, ngonjera, utenzi, nyimbo na mashairi.