NA ASIA MWALIM

UWEPO wa Makundi ya Hamasa na Itifaki nchini kumesaidia kupatikana vijana imara na wazalendo wenye kuteta maslahi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupata maendeleo na kuendelea kubaki madarakani siku hadi siku na sio kusikiliza majungu.

Mwakilishi wa Jimbo la Amani Rukia Omar Ramadhan, aliyasema hayo alipokua akifanya uzinduzi wa Kundi maalumu la Hamasa na Itifaki wadi ya Kisauni, hafla iliyofanyika Tawi la CCM Kisauni Unguja.

Alisema ni vyema kuendelezwa makundi hayo ili kujenga fursa ya Chama Cha Mapinduzi kuendelea kupata ushindi wa kishindo miaka inayokuja sambamba na kupata viongozi bora wa kuongoza ndani na nje nchi.

Aidha aliwataka vijana kuendelea kujitoa kwa ajili ya chama chao na kuacha kusikiliza maneno ya wasiopenda maendeleo ya nchi sambamba na kuhamasisha vijana wengine maendeleo yaliyopatikana kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia chama hicho.

Alieleza kujenga uimara wa kundi hilo na kuwapongeza kwa shughuli wanazozifanya kuunga mkono CCM, pia kuahidi kutoa mashirikiano kwa makundi mbali mbali ya vijana waliojitoa ili kutimiza malengo yao bila ya kujali eneo wanalotoka hivyo aliwasisitiza kutokata tamaa.