NA HAFSA GOLO
WAKALA wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali amesisitiza umuhimu wa kufanya vipimo vya vinasaba (DNA) katika kuzipatia ufumbuzi kesi za udhalilishaji.
Akizungumza na Zanzibar leo, Mkurugenzi Utawala wa wakala huo, Dk. Mwanajuma Salim Othman ofisini kwake Maruhubi, alisema vipimo hivyo vina mchango mkubwa katika ushahidi wa kesi za udhalilishaji.
Alisema serikali imetumia fedha nyingi kununua mashine hoiyo kwa lengo la kupambana na masuala ya udhalilishaji na makosa mengine ya jinai.
“Ni vyema mara ya kutokezea matokeo ya udhalilishaji watoto chini ya umri wa miaka 10 wafikishwe katika vituo vya mkono kwa mkono ndani ya saa 24 na si zaidi ya masaa 72,” alisema Dk. Mwanajuma.
Akizungumzia ufanisi wa mashine hiyo, Dk. Mwanajuma alisema kati ya Januari hadi Disema, 2021 kesi 20 za udhalilishaji wa kijinsia kwa watoto zilifanyiwa uchunguzi, watoto waliopeana ujauzito 19 na kesi za uchunguzi kwa wanandoa uthibitisho wa watoto zilikuwa tano.
Nae Mkemia wa maabara za wakala huo, Dk. Fahad Nassor, alisema kifaa hicho kina uwezo wa kukusanya sampuli tofauti yakiwemo manii, nywele za muathirika aliyefanyiwa vitendo hivyo, damu, mate, damu, nguo za ndani na za nje ambazo amevaa muhusika siku aliofanyiwa udhalilishaji.