BAADA ya miezi kadhaa ya mzozo, mivuatano na vita nchini Ethiopia, Abiy Ahmed Waziri Mkuu wa nchi hiyo ametangaza msamaha na kuwaachia huru wafungwa mashuhuri wa kisiasa akiwemo kiongozi wa upinzani Jawar Mohammed na maafisa wa chama cha upinzani cha Tigray.

Hatua hiyo imekuwa ikisifiwa na kutafsiriwa kuwa ndio mwanzo wa kupiga hatua zenye lengo la kurejesha utilivu wa kisiasa na kuandaa uwanja kwa ajili ya mazungumzo ya kitaifa.

Tangazo la kuachiliwa kwa viongozi hao, limetolewa baada ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kutoa taarifa ya mwito wa kutafuta “maridhiano ya kitaifa”.

Ikitajwa orodha ya wanasiasa waliopewa msamaha ni pamoja na wanachama kadhaa waandamizi wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF), ambao wapiganaji wao wamekuwa kwenye vita na mapigano makali na vikosi vya jeshi la serikali ya Addis Ababa tangu Novemba 2020, pamoja na viongozi mashuhuri wa upinzani kutoka jamii za Oromo na Amhara.

Jawar Mohammed na Eskinder Nega, ambao walikamatwa na kuwekwa kizuizini Julai 2020 kufuatia machafuko makubwa yaliyozuka baada ya kuuawa msanii maarufu wa jamii ya Oromo Hachalu Hundessa nae ni miongoni mwa wanasiasa waliopata msamaha huo wa serikali.

Aidha wengine ni Sebhat Nega, Kidusan Nega, Abay Woldu, Abadi Zemu, Mulu Gebregziabher na Kiros Hagos ni miongoni mwa viongozi wa Tigray waliopewa msamaha.

Wizara ya Sheria ya Ethiopia ili tamka wazi kuwa, msamaha kwa Mohammed Jawar na Eskinder Nega umetolewa ili “mazungumzo yajayo ya kitaifa yafanikiwe na yawe jumuishi”

Taarifa ya serikali ya Ethiopia imesisitiza kuwa, daima ufunguo wa umoja ni mazungumzo na kwamba, kupatiwa ufumbuzi matatizo ya nchi hiyo ni jambo linalohitajia mazungumzo jumuishi.

Habari zaidi nunua gazeti la zanzibar leo la tarehe 11 Januari,2021