Katika harakati za kuimarisha uhusiano wa kimataifa pamoja na kistretejia, nchi ya Iran inaonekana kuchukuwa juhudu kubwa za kujenga mwega kwa mataifa makubwa kama vile China na Urusi na haya yote yanajiri kutokana na diplomasi ya nchi ya Iran na mataifa ya kimagharib bado haiko vizuri.

Hivi karibuni itakumbukwa kuwa nchi ya Iran ilikubali kuanza utekelezaji wa mkataba wa miaka 25 wa ushirikiano wa kistratejia baina yake na taifa lenye utajiri mkubwa duniani ambalo ni China.

Huku ikielezwa kuwa lengo la kutiliana saini mkataba huo ni kuimarisha uhusiano baina pande mbili hizo hususan kwenye masuala ya kistretejia.

Kwa mujibu wa Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza hivi karibuni wakati akiwa mwishoni mwa safari yake nchini China kwamba:

“katika safari hiyo, pande mbili zimekubaliana kuanza utekelezaji wa makubaliano kamili ya mashirikiano ya kistratejia baina ya nchi mbili.”

Aidha akibainisha umuhimu wa makubaliano hayo, Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kuwa:

“Kuanza kutekelezwa makubaliano kamili ya ushirikiano wa kistratejia baina ya Iran na China likiwa taifa la pili kwa uchumi mkubwa duniani tena katika mazingira ambayo Marekani ingali inaendeleza  hatua zake za upande mmoja na kudumisha mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa ikifuatilia suala la kuinyima Iran haki ya kuwa na ushirikiano wa kiuchumi na dunia, kwa hakika hili linahesabiwa na Tehran kuwa ni mafanikio ya kistratejia.”

Hii inaonesha jinsi gani taifa la Iran linavyofanya juhudi katika kuimarisha siasa zake za nje pamoja na kuimarisha mahusiano kwa mataifa hayo.

Kwamujibu wa vyombo vya habari vya taifa hilo, vimeripoti kuwa, Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiisalmu ya Iran siku ya Jumatano alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Vladimir Putin wa Russia mjini Moscow ambapo pande mbili hizo zimejadili masuala ya kieneo na kimataifa.

Inaelezwa kuwa katika mazungumzo hayo, Rais Raisi ameashiria nafasi muhimu kwa Russia na Iran kwa upande wa kieneo na kidunia.

“Ufahamu wa pamoja wa nchi mbili kuhusu masuala ya kieneo na kimataifa ni msingi wa ushirikiano ya pamoja. Uhusiano wa Russia na Iran uko katika mkondo wa pamoja wa kimkakati.” alisema

Aidha Raisi amesema kipaumbele katika sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuwa na maingiliano mema na nchi jirani pamoja na waitifaki na kuongeza kuwa, “kuimarishwa ushirikiano wa Iran na Russia kutapelekea kuboreka uchumi wa nchi mbili na pia kuimarika kiwango cha usalama wa kieneo na dunia nzima.”

Kwa upande wake, Rais Vladimir Putin wa Russia alisema kuwa, hivi sasa kunatekelezwa miradi mikubwa ya maendeleo baina ya nchi mbili na kuongezwa kuwa Iran na Russia zinaendeleza ushirikiano katika nyanja mbali mbali.

Ameendelea kusema: “kwa upande wa kimataifa, tuna ushirikiano wa karibu. Kwa jitihada za nchi hizi mbili, tumeweza kuisaidia Syria kukabiliana na magaidi wa kimataifa.”

Wachambuzi wa wanaeleza kuwa mkutano wa marais wa Iran na Russia unajiri wakati ambao kumeshadidi mvuntano kati ya nchi za Magharibi na Russia hasa kuhusu Ukraine na sambamba na mazungumzo ya Vienna ya kuondolewa vikwazo haramu dhidi ya Iran.

Kwa hivyo mkutano wa Putin na Raisi una umuhimu mkubwa kwa mitazamo ya kiuchumi na kisiasa, na ni mwanzo wa msimu mpya wa uhusiano baina ya nchi mbili kwa lengo la kuimarisha ushirikiano endelevu na wa muda mrefu.

Hivi sasa Iran na Russia zinakabiliwa na vikwazo mbali mbali vya Marekani na zinapinga sera za Washington za upande mmoja na uingiliaji wa masuala ya ndani ya nchi zingine.

Kutokana na mivutano hiyo na nchi za magharibi inaonesha wazi kuwa nchi ya Iran na Russia zina maslahi ya pamoja ya kistratijia  katika uhusiano wa kisiasa, kiuchumi, kijeshi na kiusalama.

Aidha nchi hizi mbili hizi, zina mitazamo sawa katika masuala mengi ya kimataifa yakiwemo yale yanayojiri Asia ya Kati, Caucasia, Afghanistan, Yemen, Iraq na Syria katika vita dhidi ya ugaidi.

Hivyo basi ndio maana, Iran na Russia zinazingatia kwa kina uimarishwaji uhusiano wa pande zote hasa katika biashara, fedha, uwekezaji na ushirikiano wa muda mrefu katika mipango mengi ili kusambaratisha vikwazo.

Aidha kuna maslahi mengi ya pamoja ya Iran na Russia na nchi mbili zinaweza kutumia uwezo wao mkubwa katika nyanja za mafuta na gesi na pia uchukuzi wa kimataifa kupitia korido ya kaskazini-kusini.

Viongozi wa Iran na Russia katika kuimarisha ushirikiano kwa pande zote unadhamini maslahi ya kiuchumi ya pande mbili na ni chanzo muhimu cha usalama na uthabiti katika eneo sambamba na kudhamini sera za kuhusishwa pande kadhaa katika masuala ya kimataifa.

Katika mkutano wa Raisi na Putin, kumefanyika mazungumzo mapana kuhusu masuala ya pande mbili, kieneo na kimataifa na hilo linaonyesha ukaribu wa mitazamo ya nchi hizi mbili na pia azma ya kuimarishwa uhusiano wa muda mrefu.

Hossein Amir-Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuhusu mkutano huo kuwa:

“Katika mkutano huu muhimu wa kirafiki na uliodumu kwa muda mrefu mjini Kremlin, Raisi na Putin wameainisha mkondo mpya na wa kasi katika uhusiano wa Tehran na Moscow. Katika msimu mpya wa uhusiano kutakuwa na uhusiano bora. Marais wa nchi mbili wamefikia mapatano ya kuainisha ramani mpya ya njia ya uhusiano wa muda mrefu.”

Kutokana na juhudi zinazochukuliwa na Iran pamoja na taifa la Urusi inaonekana wazi kuwa ni kujenga nguvu moja baina ya serikali hizo mbili ili kuweza kuvishinda baadhi ya vikwanzo viliowekwa na nchi za Magharibi.