NAIROBI, KENYA

MACHO na masikio ya wengi sasa yanaelekezwa katika Ukumbi wa Bomas mjini Nairobi, ambapo Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi anasubiriwa kwa hamu kuu kutoa tangazo kubwa la kisiasa analofananisha na tetemeko la ardhi.

Aidha, Mudavai anatarajiwa kuzindua rasmi azma yake ya kuwania urais pamoja na ilani na jinsi vigogo wenza katika Muungano wa Kenya OKA walivyofanya awali.

Mudavadi ameahidi kutoa tangazo ambalo litatikisa miamba ya siasa za Kenya na kubadili mkondo wa mambo kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Hayo yanajiri huku mjadala mkali ukiendelea katika mitandao ya kijamii kwamba Mudavadi anapanga kuzindua muungano mpya wa Kisiasa kwa jina Kenya Kwanza Alliance KKA.