KINSHASA, DRC

MTU mmoja ameuawa huku wengine 30 wakikamatwa na maofisa usalama katika maandamano ya wakaazi wa mji wa Beni wanaoshinikiza kuondolewa hali ya mzingiro katika majimbo ya kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yaliyokumbwa na machafuko na mauaji ya mara kwa mara ya magenge ya waasi.

Sebastien Kahuma, kamisha mkuu wa polisi katika mji wa Beni alisema maandamano hayo yaligeuka na kuwa ya fujo, huku baadhi ya waandamanaji wakivamia maduka na mabenki.

Alisema polisi walilazimika kutumia nguvu kukabiliana na waandamanaji baada ya makundi ya vijana  miongoni mwa waandamanaji kufunga barabara kuu zinazoelekea katika jiji hilo la kaskazini mwa nchi.

Polisi ya DRC ilisema vijana hao walichoma moto pikipiki mbili katika barabara ya Kanzuli Beni-Mangina, na kwamba mtu mmoja ameuawa kwa kupigwa risasi na maofisa usalama.