NA HAJI NASSOR, PEMBA

WAALIMU wapya wa Chuo cha Taifa cha Zanzibar ‘SUZA’ tawi la Pemba, wamekumbushwa kujitenga mbali na matumizi mabaya ya simu za mkononi, kwani wasipokuwa makini, zinaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa maadili.

Kauli hiyo imetolewa na Mwanasheria wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba, Mohamed Hassan Ali, wakati akijibu hoja za waalim hao, kwenye mkutano wa wazi, wa kutoa elimu ya sheria, ulioandaliwa na Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria.

Alisema, sheria inaweza kumfikisha mtu yeyote mahakamani, ikiwa ataitumia simu kwa kumkashifu mwengine au kumvunjia haki zake za binadamu.

Alieleza kuwa, wapo wengine wamekua wakizitumia simu kurikodi matusi, picha chafu ambapo kwa mujibu wa sheria, hilo linaweza kuwa kosa la jinai.