SIKU chache zilizopita mke wa Rais wa Zanzibar, mama Maryam Mwinyi alizindua taasisi ya ‘Zanzibar Maisha Bora Foundation’ (ZMBF), ambapo msingi wa kuasisiwa kwa taasisi hiyo ni kusaidia changamoto mbalimbali katika jamii yetu.

Ni utaratibu wa kawaida kwa watu mashuhuri, lakini wale wenye nia ya dhati, wenye uchungu na wenye kuguswa na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii, kuunda taasisi za namna hii.

Ushahidi wa hayo ni kwamba wapo watu mashuhuri pengine kuliko mama Maryam na wana fedha nyingi katika jamii, lakini hawana wazo la kuwa na jumuia ama taasisi ya kusaidia matatizo ya jamii kwa sababu hawaguswi na changamoto hizo.

Wapo wengine katika jamii yetu wana uwezo mkubwa wa kifedha, lakini cha kushangaza sana wanahiyari wakasaidie kwenye mambo ya kipuuzi yasiyo uatuzi wa changamoto za jamii.

Kwa mujibu wa mama Maryam ambaye ni mwenyekiti wa ZMBF, taasisi hiyo inalenga kusaidia changamoto za kiuchumi hasa zinazowakabili wanawake na vijana, sambamba na kusaidia matatizo yanayowakabili watoto.

Zanzibar kama zilivyo nchi nyingi barani Afrika wanawake ndio wazalishaji wakubwa na ndio kundi lenye kutuma nguvu nyingi kwenye uzalishaji, hata hivyo kwa bahati mbaya ndio wanaokabiliwa na umasikini kwa kiwango kikubwa.

Kwa mfano, uzalishaji wa zao la mwani, inakadiriwa kuwa asilimia 80 ya wakulima wanaozalisha zao hilo hapa Zanzibar wanawake ndio wazalishaji wa zao hilo, hata hivyo kipo kilio kikubwa cha bei ndogo isiyokidhi nguvu kazi wanazozitumia.

Kupitia taasisi ya ZMBF, mama Maryam ameahidi kusaidia wanawake wanaozalisha mwani hapa nchini ili wanufaike kwa kujiongezea kipato ambacho kitasaidia kubadilisha maisha yao.