NA ASIA MWALIM

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema imeridhishwa na kasi ya utengenezaji wa boti za uvuvi inayofanywa na kampuni zilizopewa zabuni za utengenezaji wa boti hizo.

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Suleiman Masoud Makame, aliyasema hayo wakati akikagua boti za uvuvi, mwani alipofanya ziara kwenye kiwanda cha Qiro Group Company, Amani viwanda vidogo vidogo Unguja.

Waziri Suleiman alisema kazi inayofanywa na kiwanda hicho inapaswa kuigwa na kupigiwa mfano, kutokana na maendeleo makubwa yaliyopatikana kwa muda mfupi.

Waziri huyo alisema katika kipindi kifupi kilichopita kampuni hiyo ilikabidhiwa jukumu la kutengeneza boti 250, ambapo hadi sasa wametengeneza zaidi ya boti 120.

Alifahamisha kuwa serikali ilitangaza zabuni kwa ajili ya kutengeneza boti za mwani zenye urefu wa mita tano na boti za uvuvi, ili kuona dhana ya uchumi wa buluu na uvuvi inafikiwa katika maeneo yote ya Zanzibar.

Hata hivyo, alibainisha kuwa katika maeneo yote ya utengenezaji boti waliyotembelea amefaririjika kuona muwekezaji huyo amefanya vizuri pia amechukua idadi kubwa ya zabuni ukilinganisha na wawekezaji wengine.