HAFSA GOLO NA MARYAM HASSAN

WAZIRI wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Mohamed, amesema riba na vitendo vya hadaa ni miongoni mwa sumu inayochangia kuviua vyama vya ushirika wa kuweka na kukopa (SACCOS) vinazoanzishwa nchini.

Dk. Khalid aliyasema hayo wakati wakati akifungua mkutano  mkuu wa nne wa ushirika wa Mamlaka Sacocos ya Viwanja vya Ndege iliyofanyika katika tawi la CCM, Kiembesamaki.

Alisema vitendo hivyo hupelekea kupoteza malengo yenye kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa vyama vya ushirika na  wanasacos na hatimae  kutofikia  ndoto zao walizojiwekea.

Aidha waziri huyo aliwashauri wanunuzi wa vifaa na mahitaji mengine katika sacos hiyo kuhakikisha hawaendi  kinyume na sheria za manunuzi wala kujihusisha na vitendo hivyo ambavyo vinachangia kubeza maendeleo.

“Miradi mingi ikiwemo maduka yalioanzishwa na vikundi vya ushirika huko nyuma ilikufa kutokana na ukiukwaji wa sheria na taratibu pamoja na wanunuzi kufanya vitendo vya hadaa,” alisema.