NA ZAINAB ATUPAE
KOCHA Mkuu wa KMKM, Ame Msim, amepinga taarifa zinazungumzwa kwamba walifanya mazungumzo ya kuwauzia mechi Uhamiaji juzi.
KMKM ilipokea kichapo cha mabao 2-1 mbele ya Uhamiaji katika
mchezo wa Ligi Kuu ya Zanzibar ulichezwa uwanja wa Amaan.
Akizungumza na gazeti hili, Kocha huyo, alisema, hakuna mazungumzo yaliofanywa kati yao na Uhamiaji yaliolenga kuuziana mechi na walifungwa kutokana na kuzidiwa kimchezo.
Alisema sababu kubwa ya kupoteza mchezo huo ni baada ya wachezaji kucheza kwa kujiamini na huko ndiko kulikowaponza na kuzikosa pointi tatu walizozitegemea.Kocha huyo, alisema, kupoteza mchezo huo kwao imekuwa pigo, lakini, wanajipanga na mchezo dhidi ya Zimamoto unaotarajiwa kuchezwa Mei 17.
“Hatukutarajia, lakini, tumeyakubali matokeo na tunakwenda kujipanga ili kuona hatufanyi maakosa kwenye mechi jayo”.
“Mchezo ulikuwa mgumu zaidi tulivyotegemea, tulizidiwa dakika za mwisho na kupoteza nafasi”.
Hata hivyo, alisema, bado wanayo nafasi ya kutetea ubingwa kutokana na kubakiwa na mechi nne na kwamba kinachotakiwa ni kushinda mechi mbili ili kutawazwa mabingwa.”Malengo yetu yanabakia ni kutetea ubingwa wetu, tunaongoza ligi na tunakiwa kushinda mechi mbili tu”, alisema.