KWA mujibu wa kumbukumbu zetu mnamo Machi 8 mwaka 2022, bweni la wanafunzi wanawake katika skuli ya Utaani ambao walikuwa kwenye maandalizi ya mitihani wa kidato cha sita liliteketea moto.

Katika tukio hilo la kusikitisha mbali ya jengo kuharibika vibaya, lakini pia vifaa muhimu vya wanafunzi hao ikiwemo nguo, madaftari, vitabu, magodoro yalikwenda na maji.

Tunashukuru katika tukio hilo hakuna mwanafunzi aliyefariki duniani, hata hivyo kwa fadhaa za wanafunzi na papatu papatu ya kuokoa maisha yao wapo waliopata msongo wa mawazo.

Taarifa rasmi ya moto huo tuliyoelezwa baada ya uchunguzi wa kina uliofanywa na mamlaka husika, tuliambiwa kuwa moto ulioteketeza bweni hilo chanzo chake hitilafu ya umeme.

Wakati tukitafakari tukio la Utaani, wiki chache zilizofuata kulitokea tukio jengine la kuungua bweni la wanafunzi wa kiume katika skuli ya Madungu iliyopo Chakechake Pemba.

Tukio jengine la kuungua bweni la wanafunzi wa kike limejirejea tena mnamo Mei 16 mwaka 2022 katika skuli ya Ufundi iliyopo Kengeja mkoa wa Kusini Pemba.

Katika tukio la moto skuli ya Ufundi Kengeja, kilichobahatika kuokoa ni roho za wanafunzi 96 waliokuwa wakiishi katika bweni hilo kwa shughuli za faradhi ya lazima ya kujitafutia elimu.