WAFANYAKAZI iwe kwenye sekta ya umma ama binafsi,  ni watu muhimu sana serikalini na kwenye jamii kwa ujumla, ambapo umuhimu wao unatokana na kwamba wao ndio wasimamizi na watekelezaji wa utoaji huduma mbalimbali kwa wananchi.

Kila inapofika Mei Mosi wafanyakazi na watumishi masikio yao huyaelekeza kwenye hotuba za viongozi wa nchi ambao mara nyingi huwa ndio wageni rasmi kwenye sherehe za wafanyaakazi duniani kusikiliza je! wakuu hao wameongeza maslahi yoyote je! Wametoa ahadi yoyote?

Katika sherehe za wafanyakazi duniani za mwaka 2022, historia mpya imeandikwa nchini Tanzania ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, wamevisikia vilio vya wafanyakazi.

Kwa upande wa Rais wa Jamhuri yeye ameridhia kupandishwa mshahara kwa asilimia 23.3, ambapo ametenga kiasi cha shilingi trilioni 9.7 kwa ajili ya kugharamia malipo ya mishahara ya watumishi wote katika serikali kuu, serikali za mitaa, taasisi na wakala za serikali.

Kwa upande wake, Dk. Mwinyi ametangaza kuongeza mshahara kuanzia kima cha chini kwa asilimia 15.9 na kuendelea, ambapo kwa ujumla kiasi cha shilingi bilioni 153 kwa mwaka zikitengwa kugharamia ongezeko hilo kwa wafanyakazi wote wa umma.

Ongezeko la mshahara lililotangazwa na Dk. Mwinyi limepangwa kwenda kuondosha maung’uniko ya muda mrefu hasa kwa wafanyakazi wasio na elimu, ambapo mara nyingi kila ongezeko la mshahara linapofanywa kundi hili haliangaliwi kwa upana wake.

Aidha katika ongezeko hilo lililotangazwa Rais wa Zanzibar, kutazingatia utumishi wa muda mrefu, wafanyakazi kupangwa madaraja na vyeo vya wafanyakazi kwa mujibu wa miundo ya utumishi wa umma.

Tumezoea kuona mishahara inapopandishwa elimu huwa ndio kigezo kikubwa kwa maana ya kwamba ukianzia digirii ya kwanza, ya pili na tatu mambo huwa safi sana, huku wenye uhaba wa elimu na wenye uzoefu hawazingatiwi.