NA MWANDISHI WETU

ILI nchi yoyote duniani iweze kufikia malengo ya kimaendeleo, haina budi kuwa na mipango bora katika matumizi ya rasilimali zake, ili kuhakikisha zinakuwa endelevu na kuleta tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kwa kipindi kirefu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imekuwa ikilipigia kelele suala la usimamizi mzuri wa rasilimali zake za ardhi, kwa kuamini kuwa ndio chimbuko la maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Kutokana na rasilimali hiyo, nchi inaweza kufikia hatua kubwa ya maendeleo kwa haraka, kupitia sekta mbali mbali, kama vile kilimo, uvuvi, mafuta na gesi asilia, pamoja na Uwekezaji katika sekta ya viwanda na biashara.

Lakini pia kutokana na ardhi, pia kuna rasilimali muhimu za mchanga na misitu au Hifadhi za Taifa, ambamo ndani yake, sekta ya utalii imejikita. ‘‘Kwa vyovyote vile ardhi ndio kila kitu’’, katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya binadamu.

Kwa kuzingatia dhana ya ardhi kuwa ndio rasilimali muhimu zaidi katika maisha ya kila siku ya binaadamu na ustawi wa Taifa letu, tulitegemea wale wote waliokabidhiwa jukumu la usimamizi wa rasilimali hii, wangekuwa makini, waadilifu na wanaojali dhima na dhamana walizokabidhiwa na Taifa.

Ni vyema ikakumbuka kuwa maendeleo ya kweli ya Wazanzibari, iwe yatokanayo na chakula, malazi au vyenginevyo, yatatokana na rasilimali nyeti ya ardhi.

Katika dunia ya leo, nchi kadhaa duniani zilizoendelea na zile zinazoendelea, zimeweka mazingatio na kutambua thamani ya kila robo ya hekta ya ardhi waliyonayo.

Kwa muktadha huo ni wazi kuwa kila eneo dogo la ardhi tayari limekewa mipango mizuri ya kuendelezwa, kutegemea na aina ya mradi au kazi iliyopangwa.