DUNIA imeweka siku mahususi ya kupinga matumizi ya tumbaku na bidhaa zake ambayo ni Mei 31 ya kila mwaka, ambao shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), iliteua siku hiyo kwa kutambua athari za janga la matumizi ya tumbaku zinavyozidi kuongezeka na kuangamiza watu.

Kwa mujibu wa takwimu za WHO, athari zinaotokana na matumizi ya tumbaki na biadhaa zake huua kiasi cha watu milioni sita kila mwaka duniani kote wanaovuta na wengine 600,000 wanaovutishwa moshi wa tumbaku.

Kila baada ya sekunde 10, mtu mmoja hufariki duniani kutokana na maradhi yanatokana na matumizi ya bidhaa za tumbaku, ambapo asilimia 70 ya watumiaji wa tumbaku wanatoka katika nchi zinazoendelea.

Wataalamu wa maswala ya afya wanabainisha kuwa ifikapo mwaka 2025 vifo vinavyotokana na matumizi ya tumbaku vitaongezeka kwa asilimia 70 na ifikapo mwaka 2030 watu milioni milioni 10 watapoteza maisha   kutokana na uvutaji wa sigara.

Kwa takwimu hizi jamii inapaswa kujitahmini na kuchukua tahadhari ili kuepukana na athari za matumizi ya tumbaku ambapo wataalam wanabainisha kuwa athari za bidhaaa za tumbaku si kwa mtumiaji tu bali humpata mtu aliye karibu na anayetumia bidhaa za tumbaku.

Madhara ya matumizi ya bidhaa zinazotokana na tumbaku ni mengi ikiwa ni pamoja na kuwa ni kichocheo cha maradhi yasiyombukiza kama shinikizo la damu, saratani na kisukari.

Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 47 ya wagonjwa wanaougua maradhi ya kansa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili inatokana na matumizi ya bidhaa za tumbaku.

Tumbaku inaathiri ubongo na kusababisha ugonjwa wa akili, upungufu wa nguvu za kiume, matatizo katika njia ya hewa ikiwemo pumu sugu na kuathiri mapafu na hatimae kushindwa kupumua.

Bidhaa za tumbaku huathiri ngozi, kupata ngozi kavu na hatimae saratani ya ngozi, pia huathiri kinywa, huharibu meno na kutoa harufu mbaya mdomoni na kusababisha karaha.

Maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya kupinga matumizi ya tumbaku duniani hapa Zanzibar yameanza kwa kuielimisha jamii juu ya athari ya matumizi ya tumbakuna bidhaa zake.

Kwa watumia tumbaku na bidhaa zake, huu ni wakati wa kutafakari na kuchuka hatua muafaka ambazo ni kuacha kabisa matumizi ya tumbaku na bidhaa zake.

Tutashangaa sana baada ya kuizona athari hizo zote zilizobainishwa kutokana na tafiti za wataalamu kuwaona watu katika jamii wanaendelea kutumia tumbaku na bidhaa zake.

Hebu jiulize kama utaendelea kutumia tumbaku na bidhaa zake na ukafika wakati umepata maradhi ambayo chanzo chake kimetokana na matumizi ya tumbaku si utakuwa sawa na mtu aliyejidhulumu mbele ya Mwenyezi Mungu?

Umefika wakati wa kila mwana jamii atafakari athari za matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, lakini jamii ihakikishe inasimama kupambana na matumizi ya dawa hizo.