NA KHAMISUU ABDALLAH

WAZIRI wa Nchi Ofisi, Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Saada Mkuya Salum, ameitaka Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) kuzingatia sifa za kitaaluma wanapotoa ajira za mkataba badala ya uenyeji.

Kauli hiyo aliitoa wakati akizungumza na uongozi wa bodi hiyo katika ofisi za ZRB Mazizini na kueleza kuwa watu wengi Zanzibar wamejenga dhana ya uenyeji katika masuala ya ajira bila ya kuzingatia sifa alizonazo.

Hivyo alimsisitiza Kamishna wa bodi hiyo, Yussuph Juma Mwenda kutoruhusu mtu yoyote katika jambo hilo badala yake kutafuta watu watakaoingia katika ajira hizo na kuongeza ufanisi.

“Kama kuna mtu ambae ana jamaa yake basi amwambie kabisa kama ajira hizi hazitaki uwenyeji wa mtu bali wanaotakiwa ni wale wenye sifa na kamapata kwa nguvu zake mwenyewe hakikisha mtu anaingia katika ajira kwa uwezo na utashi wake asije mtu akamleta ndugu yake ulisimamie hili,” alisisitiza.

Hata hivyo, alisema jambo hilo litajenga uthubutu kwa vijana wa Zanzibar katika kutafuta ajira kwa nguvu zao wenyewe bila ya kumtegemea mtu.