VIJANA ndio nguvu kazi ya uzalishaji katika taifa lolote, kutokana na umri, nguvu, maarifa, udadisi,ugunduzi na vipaji vyengine walivyonavyo ambavyo ni vigezo muhimu katika kuendana na kasi ya ushindani wa ulimwengu wa leo.

Taarifa za Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Taifa (NBS, 2020) asilimia 64 ya makadirio ya idadi ya watu ni kundi la vijana, kati ya hao vijana walio kati ya umri wa miaka 15 hadi 35 ni asilimia 34.

Pamoja na hayo, vijana wanakabiliwa na changamoto lukuki zinazoweza kuharibu mustakabali wa maisha yao binafsi na kwa taifa kwa ujumla, mfano kuongezeka kwa matumizi ya madawa ya kulevya, kuongezeka kwa mmomonyoko wa maadili kutokana na athari za utandawazi, ukosefu wa elimu bora na ujuzi wa kuweza kujiajiri, ushirikishwaji mdogo katika nafasi za maamuzi na uongozi, na wimbi kubwa la vijana wasio na ajira ambalo mfumo wa elimu unaweza kuwa umechangia.

Dhana iliyojengeka ya kusoma ili kuajiriwa inachangia tatizo la ukosefu wa ajira, kundi kubwa la vijana waliopita katika mfumo wa elimu wanakuwa tegemezi baada ya kuhitimu masomo yao kusubiri fursa za kuajiriwa haswa katika sekta mbalimbali za umma serikalini, jambo hili limekuwa ni ndoto kwa vijana wengi takribani kipindi chote cha miaka 15 wakiwa masomoni kuanzia sekondari hadi chuo kikuu.

Ni ukweli usiopingika kuwa sio wote wanaoweza kupata fursa ya kuajiriwa ikiwa ni serikalini au hata katika mashirika au taasisi za sekta binafsi kutokana na kuwa nafasi za ajira ni chache ukilinganisha na idadi ya wahitaji na kila mwaka wahitimu wanaongezeka.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la utafiti REPOA ya mwaka 2019, takribani vijana milioni 1 wanahitimu kila mwaka kutoka taasisi mbalimbali za kielimu huku idadi ya ajira zinazozalishwa kutoka serikalini na sekta binafsi ni 250,000, kwa wastani kila mhitimu anatumia miaka 5.5 kutafuta ajira.

Hali kadhalika mtaala wa elimu unaotumika unaweza kuwa pia msingi wa tatizo kwa sababu unapelea kuwajengea maarifa ya msingi na uweledi kwa vijana wanaopita katika mfumo wa elimu. Kama tunavyojua mtaala wa elimu ni kama mfumo wa uzalishaji katika kiwanda, unaweza kuchakata malighafi ambayo ni mwanafunzi tangu hatua za awali za uzalishaji akiwa madarasa ya chini mpaka kufikia zao la mwisho baada ya kuhitimu chuo kikuu.

Vijana wengi wahitimu wanaonekana kukosa uweledi au maarifa ya msingi yanayoweza kuwasaidia hata wenyewe kujiajiri au kuwajengea sifa nzuri za kuwezesha kuajiriwa, ni lazima ifahamike kuwa haitegemewi mwanafunzi aliehitimu karibuni awe na maarifa makubwa ya kitaalamu, bali awe na msingi mzuri wa alichokuwa anajifunza kwa takribani kipindi cha muongo mmoja na nusu alipokuwa shuleni.

Kwa hali ya sasa si ajabu kumkuta kijana mhitimu akiwa hakumbuki chochote katika takhasusi aliyosoma, huku wengi wakiwa na ari na hamasa ndogo ya kujifunza, ishara inaonesha vijana wengi waliohitimu ni kama walikuwa na bidii kubwa ya kusoma na kujibu mitihani tu.

Kwa vipimo hivi vichache inatosha kuonesha kuwa kuna haja si ndogo ya kufanya marejeo ya mitaala inayowafunda vijana wetu wakiwa mashuleni ili badae kupata matokeo mazuri.

Mitaala yetu pia haisisitizi sana elimu ya usajiriamali, pamoja na kuwepo kwa mlolongo wa masomo kadhaa lakini bado katika taasisi au mashule mengi hakuna somo la ujasiriamali, jambo hili lingeweza kusaidia kujenga uwezo wa kuajiamini na utayari wa kujitegemea kwa kijana tangu akiwa mdogo na imtamsaidia kujitayarisha kupambana na mazingira yake mara baada ya kuhitimu.

Inaaminika kuwa hata mbuyu ulianza kama mchicha, badala ya kuwazogoa vijana wahitimu na maneno ya kuwakejeli na kuwasukumiza katika njia ya kujiajiri, kuna haja ya kuwajengea utayari huo wa kiakili na kutambua fursa zilizopo kupitia mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali tangu wakiwa wadogo shuleni.

Bado kwa kiasi kikubwa pia hatuipi umuhimu mkubwa nafasi ya elimu ya ufundi na mafunzo ya amali, ipo dhana iliyozoeleka miongoni mwetu kuwa mara nyingi wanaokwenda katika vyuo vya ufundi kupata mafunzo ya amali ni kundi la vijana au wahitimu walioshindwa kuendelea na elimu ya sekondari au hawana sifa za kujiunga na vyuo, ingawa kiuhalisia haitakiwi kuwa hivyo.

Maendeleo ya kasi katika nchi za Uchina, Vietnam, Laos, Thailand na nyenginezo kutoka Kusini Mashariki mwa Bara la Asia yamechagizwa na msisitizo mkubwa wa serikali kuwekeza katika vyuo vya kati vya ufundi kwa kuweka miundombinu ya kutosha, mitaala, vifafa vya kujifunzia, teknolojia na utaalamu, kupitia vyuo hivyo makundi ya vijana wengi wameweza kupata maarifa ya utaalamu na matokeo yake kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi na ufanisi.

Hatua kama hizo zimechukuliwa katika nchi za Scandinavia kuwekeza katika vyuo vya maendeleo ya jamii (Folk development College FDCs), mfano nchini Sweden mfumo wa elimu mbadala wa Folkbildning ambapo ndio kwa muda mrefu umeanzishwa umesaidia kulikomboa kundi kubwa la jamii ikiwemo na vijana kwa kuwapa mafunzo, maarifa na ujuzi wa fani mbalimbali ili kujiendeleza.

Kwa hapa kwetu serikali inapaswa kulitazama hilo kwa jicho la upekee na inaweza kutumia fursa hiyo kuwekeza miundombinu ya kujisomea katika vyuo vya namna hiyo,  kimkakati inaweza kutumika kama moja ya njia za kupambana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana.

Vilevile, kisera jambo hilo linaweza kuambatanishwa na mkakati wa  kufikia uchumi wa buluu, kwa kuweka mafunzo ya fani mbalimbali zitakazo wafunza vijana kutambua fursa zilizopo katika sekta za uchumi wa buluu na namna ya kuzitumia, mfano mafunzo ya uvuvi wa kisasa, uzalishaji wa mwani, uchakataji na uhifadhi, utunzaji wa vyakula bahari na mengine.

Pamoja na hayo, Kupitia mfumo wa elimu pia vijana pia wangepewa mafunzo ya kifedha, namna ya kutunza fedha na kuweka rikodi za mahesabu ili kuwasaidia kuaminiwa na taasisi za kifedha, kundi kubwa la vijana bado ni vigumu kuaminiwa katika taasisi za kifedha kwa mfano kupata mikopo ya usaidizi na mengine.

Kuendeleza michezo na kuweka mazingira ya kuendeleza vipaji mashuleni pia itasaidia, michezo ni sehemu ya ajira kwa kundi kubwa la vijana kwa sasa, kuweka akademi za michezo na mazingira rafiki katika taasisi za kielimu inaweza kusaidia kupunguza kasi ya kundi la vijana wahitimu wasio kua na ajira.

Kwa mukhtadha huo basi, vijana ni kundi muhimu linalochangia maendeleo ya taifa ikiwa litajengewa uwezo na kuwekewa mazingira Rafiki ya kujiendeleza, lakini ni kundi linaloweza kuleta changamoto kubwa kama litapuuzwa na kusahauliwa.