OUAGADOUGOU, BURKINA FASO

IDADI ya watu waliopoteza maisha kufuatia mashambulizi ya wanamgambo nchini Burkina Faso katika mji wa Seytenga imeongezeka na kufika 86 baada ya miili zaidi kupatikana.

Taarifa ya serikali ilisema kikosi maalumu kilichotumwa katika mji huo wa kaskazini kimegundua miili katika eneo la mapigano na kuongeza kuwa uchunguzi kuhusu hujuma hiyo unaendela.

Usiku wa Juni 11-12, waasi walishambuliwa Seytenga na kuua idadi kubwa ya raia.

Rais Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Dambia ambaye anaongeza utawala wa kijeshi alitembelea eneo la tukio na kuapa kukabiliana na waasi hao.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali hujuma hiyo ya magaidi nchini Burkina Faso ambapo ametoa wito kwa mamlaka za Burkina Faso kufanya juhudi zote kubaini wahusika na kuwafikisha mbele ya sheria.

Zaidi ya watu milioni 1.9 nchini Burkina Faso, wakiwemo wanawake, wanaume na watoto ni wakimbizi wa ndani kutokana na ukosefu wa usalama kwenye taifa hilo la Afrika Magharibi.

Magaidi wanaotekeleza hujuma Burkina Faso wanaaminika kuwa wametoka nchi jirani ya Mali ambayo nayo pia wiki za hivi karibuni imeshuhudia ongezeko la hujuma za kigaidi.

Mtu mmoja kati ya watano anahitaji msaada wa kibinadamu nchini Burkina Faso wakati huu ambapo ombi la mwaka huu la kibinadamu la dola milioni 591 la kufanikisha operesheni za kiutu limefanikishwa kwa asilimia 15 pekee.