MOGADISHU, SOMALIA

JESHI la taifa la Somalia lilisema kuwa lilifanya operesheni dhidi ya kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye muungano na al-Qaeda katika eneo la kati la Hiran, na kuua takriban magaidi 12 wa kundi hilo la magaidi.

Operesheni hiyo iliyoendeshwa na askari wa kikosi maalumu jeshini ilifanyika karibu na mji wa Mataban katika eneo la kati la Hiran mwishoni mwa Jumapili.

Brigedia Jenerali Odowa Yusuf Rageh, kamanda wa jeshi la taifa la Somalia aliyezungumza na redio ya jeshi, amethibitisha operesheni hiyo, akisema lengo kuu ni kuharibu maficho ya magaidi na kuzuia njama zao.

Alisema kuwa wakati wa operesheni hiyo, jeshi liliharibu kambi ya al-Shabaab huko Qabdho nje kidogo ya Mataban, ambapo magaidi wa al-Shabaab walikuwa wakipora pesa kutoka kwa watu wa eneo hilo.

Hayo yanajiri siku kadhaa baada ya Rais mpya wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud kuahidi kukabiliana na ugaidi katika nchi hiyo iliyokumbwa na mzozo, huku pia akiiomba jamii ya kimataifa iisaidie nchi hiyo dhidi ya tishio la baa la njaa.

Rais Mohamud alisema hayo wakati wa hafla ya kuapishwa kwake na kuahidi kuibadilisha Somalia kuwa nchi ya amani na kurekebisha uharibifu uliosababishwa na migogoro ya kisiasa ya miezi kadhaa.

Jeshi la Somalia linashirikiana na Askari wa Kikosi cha Mpito cha  Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika (ATMIS) katika kukabiliana na magaidi hao wa al-Shabab.

Kuna askari wapatao 20,000 kutoka Uganda, Ethiopia, Burundi na Kenya wanaohudumu katika kikosi hicho.