MWALIMU Waleed huwa na kawaida kila siku ya Ijumaa baada ya kula chakula cha mchana hujipumzisha sebuleni na kuwakusanya mkewe Bi Nihfadhi na watoto wake, Abdul, Kamilya na Rawhiya na huwahadithia yale aliyoyapata katika khutba ya Ijumaa ya siku ile.

Mwenendo huu mzuri aliuiga kutoka kwa marehemu baba yake, na akauendeleza mwenendo huo kwani aliiona faida yake naye akauchukulia kuwa ni wajibu wake wa kufikisha elimu kwa watu wake wa nyumbani.

Ijumaa hii, kama kawaida baada ya familia ya Mwalimu Waleed kukusanyikia sebuleni kusubiri kile baba yao alichokipata kwenye khutba ya Sala ya Ijumaa, Mwalimu Waleed alianza kwa kusema kwa mshangao KWA NINI NISIHIJI MWAKA HUU! Mkewe Bi Nihfadhi alionekanwa kushtuka kidogo baada ya kuisikia kauli hiyo na kumgeukia mumewe ambaye yeye alikuwa akiwatizama watoto wake. Naam! Ilimtoka Bi Nihfadhi, na kuuliza: “hiyo ndo mada ya khutba ya leo”? Mwalimu Waleed allijibu: “hapana mke wangu, mada ya khutba ya leo ilikuwa ni FADHILA ZA IBADA YA HIJJA. Mbona umeshtuka Mama Kamilya”? Mwalimu Waleed aliuliza. Bi Nifadhi alijibu kwa kusema:

“Hapana Baba Abdul sijashtuka ila nilishangaa kidogo kwani ninavyofahamu mie kwenda kutekeleza ibada ya Hijja mpaka uwe na uwezo, Namshukuru Mwenyezi Mungu rizki yetu tunapata na chejio hakitupigi chenga ila hayo mamilioni ya kwendea Hijja siyaoni humu ndani”.

Mwalimu Waleed alisema huku akitabasamu: “nimeraghibika sana baada ya kuzisikia fadhila za kutekeleza ibada ya Hijja isitoshe si unafahamu kwamba hivi sasa nipo katika likizo ya kustahafu, nitatumia sehemu ya kiinua mgongo changu niende kuondosha uwajibu wangu huo ambao ni nguzo ya tano ya dini yetu”. Aliongeza kusema:

“Nitakapopata kiinua mgongo changu nitakuwa tayari nimeshapata uwezo na sitokuwa na udhuru wala sababu ya kutokwenda kutekeleza ibada ya Hijja, na kwa vile bado afya yangu ni nzuri ni vyema nikenda kutekeleza ibada ya Hijja mwaka huu, kwani hakuna anojuwa yajayo”.

Rawhiyya mtoto wa mwisho wa Mwalimu Waleed ambaye anapenda kucheza cheza na kumfanyia mas’hara sana baba yake, alirukia kwa kumuuliza baba yake: “Dady kama ukifa je kabla ya hiyo Hijja ya mwaka huu itakuwaje”? Mwalimu Waleed alicheka na kusema: “miye tayari nishatia nia mwanangu na Muislamu hulipwa kwa mujibu wa nia yake, na nia ya Muumini ni bora kuliko vitendo vyake.

Nawausia wanangu pamoja na mke wangu pindi Qadari ya Mwenyezi Mungu itakapotokea na akanikhitari kama alivouliza Rawhiyya, hakikisheni ikiwa bado sijafanya malipo, mnakwenda kulipia kwenye Taasisi ili nikafanyiwe Hijja kwani nimesikia matangazo kuwa zipo Taasisi zinawahijia watu kwa bei pungufu, na kama nishalipa nendeni kwenye Taasisi niliyolipia muwape taarifa na kuwaambia wakate fedha za kwenda kuhijiwa na zilobaki wakupeni nyie ziingizwe kweye tarika na zirithiwe”.

Kamilya alisema huku akimtazama Rawhiyya: “Dady Mwenyezi Mungu atakujaalia umri mrefu na utakwenda kuhiji mwenyewe kwa miguu yako” wote waliitikia kwa pamoja kama waloambizana “aamiyn”.

Abdul muda wote alikuwa amekaa kimya akisikiliza, ghafla kama aliyezunduka kutoka usingizini alimwita baba yake, “Mzee! samahani, naona leo bado hujatupa yaliyozungumzwa kwenye khutba”. “Ah! Si unaona walivonishughulisha mamaako na ndugu zako kwa masuala yao”. Mwalimu Waleed alisema:

“Haya kwanza kabla ya kuanza kukuelezeeni yaliyosemwa kwenye khutba, je kuna mtu yeyote bado ana suala”? Mwalimu Waleed aliuliza. Abdul alijibu: “Ukweli Mzee mimi nilikuwa na hamu ya kujuwa hizo fadhila za Hijja hata ukashajiika na kudhamiria kwenda kutekeleza ibada ya Hijja mwaka huu, lakini kwa vile umetowa fursa tukuulize, nami naomba kuuliza”.

Mwalimu Waleed alimruhusu mwanawe Abdul kuuliza. Abdul aliuliza: “Mzee uliniahidi nikipasi kidatu cha nne utaninunulia Honda click nami nimepasi je ahadi yako bado ipo au imevunjwa na safari yako ya Hijja”?

Kabla hajajibu Bi Nihfadhi mke wa Mwalimu Waleed naye alirukia: “Na mimi uliniahidi kiwanja changu cha urithi utanisaidia kuanza ujenzi vipi”? Mwalimu Waleed aliwajibu kwa upole na kuwaambia: “ahadi zangu ziko pale pale namuomba Mwenyezi Mungu anipe uwezo isipokuwa ahadi hizo nitazitekeleza kwa mujibu wa umuhimu na uzito wake, si mnajuwa kwamba kuhiji ni nguzo na ni lazima”? Walijibu: “naam tunajuwa”.

“Hivyo nitaanza na hilo la kukamilisha nguzo na baadae nitayatekeleza yatakayobakia, msiwe na wasi wasi”. Alimalizia Mwalimu Waleed. “Naam kuna mwengine mwenye suala”? Mwalimu Waleed aliwauliza wanafamilia yake waliokuwepo ukumbini. “Naam lipo baba Abdul”.

Bi Nihfadhi alijibu. Akauliza baada ya kuruhusiwa kwa kutikisiwa kichwa na mumewe. “Jitihada gani utafanya ili uzipate pesa zako za kiinua mgongo kabla ya kufika muda wa mwisho wa kulipia”?, “Kwani nimemsikia shoga yangu Ukhti Mwana huyu jirani yetu ambaye mumewe ana Taasisi ya kusafirisha Mahujaji, akisema kwamba mtandao wa kieletroniki wa shughuli za Hijja, utafungwa mwishoni mwa mwezi wa Shaabani.”

Mwalimu Waleed alijibu kwa kusema: “Katika jamii yetu bado watu wa kheri wapo na wapo wanaofahamu kwamba kumsaidia mtu kwenye jambo la kheri nawe unapata ujira mkubwa, na watu hao wapo katika sehemu nyingi ambazo mwenye kwenda Hijja anapitia na kumuwepesishia mambo yake, kama vile wafanyakazi wa sehemu ya kutengeneza viinua mgongo, Wafanyakazi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, Wafanyakazi wa Idara ya Uhamiaji,  Wafanyakazi wa Idara ya Chanjo hata baadhi ya Wafanya biashara.

Nimesikia kuna mmoja ukitaka picha za kuombea viza ya Hijja ukenda dukani kwake unapigwa bure bila ya kulipa chochote. Kuna mwengine anasaidia vifaa kadhaa kwa mahujaji, kama viatu, sabuni, kanga, sahani n.k.

Hivyo kuhusu jawabu la suala lako, utakapokamilisha taratibu na kuwa na uthibitisho wa kujiandikisha kwenda Hijja, Wafanyakazi wa kule kunakotayarishwa viinua mgongo wanakufanyia wepesi kupata kiinua chako mgongo mapema. Mwenyezi Mungu awajaze kheri,  Aamiyn. Haya kaeni sawa nianze kukusimulieni khutba ya leo”.

“Khutba ya leo imezungumzia Fadhila za Hijja na Sheikh Mohammed alizifafanuwa kwa ufasaha huku akitolea ushahidi wa aya za Quran na hadithi za Mtume Muhammad, “Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam” walimsalia Mtume kwa sauti kwa pamoja isipokuwa Rawhiyya yeye alikaa kimya. Mwalimu Waleed alimgeukia Rawhiyya na kumwambia kwa kumkumbusha, mbona hujamsalia Mtume umesahau kuwa Mtume amesema bakhili ni yule ninayetajwa mbele yake na asinisalie? Rawhiyya naye akamsalia Mtume peke yake kwa sauti ya chini. Baadae akaendelea kuwaelezea yaliyozungumzwa kwenye khutba kuhusu fadhila za ibada ya Hijja. Alianza kwa kuwaambia, “Sheikh Mohammed alianza kwa utangulizi”:

Hijja ni nguzo tukufu kati ya nguzo tano za Kiislamu, Mwenyezi Mungu ameifaradhisha kwa mwenye uwezo, mara moja tu katika umri wake. Ibada hii ina fadhila nyingi mno, baadhi ya hizo:

Ni katika amali bora ya mja kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, baada ya Kumuamini Mwenyezi Mungu na kupigana Jihadi, Hijja itakayokubaliwa haina malipo isipokuwa Pepo.

 

Fadhila nyengine ni pamoja na Mwenye kuhiji husamehewa dhambi zake zote na huwa safi kama siku aliyozaliwa na mama yake na kuhiji kwingi kunazuwia ufukara na hufuta madhambi.

 

Aidha fadhila za mwenye kwenda Hijja anakirimiwa na Mwenyezi Mungu na mwenye kuhiji hukubaliwa dua yake na hupewa anachokiomba.

 

Alizitaja fadhila nyengine kuwa ni pamoja na kila khatua anayopiga mwenye kuhiji huandikiwa thawabu na kufutiwa dhambi.

 

Pia fadhila nyengine ni Kwenda mbio baina ya Safaa na Marwa kama uliyeacha huru watumwa kadhaa sambamba na kusamehewa madhambi yule atakayeombewa msamaha na mwenye kuhiji.

Fadhila nyengine alizozitaja ni pamoja na mwenye kuhiji anaposimama kwenye kiwanja cha Arafa, Mwenyezi Mungu hujifakharisha kwa Malaika, kila kijiwe anachorombea Hujaji kwenye Jamarat husamewa madhambi makubwa.

 

“Kila unywele anaounyoa Hujaji huandikwa thawabu na hufutiwa dhambi na mwenye kuhiji huombewa dua na Malaika, ambapo pia mwenye kuhiji huachwa huru na Moto”, alizitaja fadhila hizo.

 

Sambamba na fadhila hizo, lakini alizitaja fadhila nyengine kuwa ni pamoja na mwenye kuhiji na Hijja yake ikakubaliwa hukingwa na Shetani na vitimbi vya Mashetani, hijja inafuta dhambi zilizopita.

 

Aidha fadhila nyengine ni kulibusu jiwe jeusi kwenye Alkaaba ambalo kuna Imani kuwa humuombea mja Siku ya Kiama, Kuomba dua na kutia nia njema wakati wa kunywa maji ya zamzam Allaah hukupa ulilolinuwia.

 

Pia Ibada ya Hijja hufanywa katika masiku ambayo amali njema kuifanya ndani ya  masiku hayo ni bora na inapendwa zaidi na Mwenyezi Mungu kuliko kuifanya katika masiku mengine yasiyokuwa hayo hata kama itakuwa ndani ya mwezi wa Ramadhani.

 

“Kusali ndani ya Msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) Madina sala moja tu, unalipwa kama uliosali sala elfu moja katika misikiti mingine isipokuwa Msikiti Mtukufu wa Makka na Msikiti wa Baytul Maqdis. Yaani sala moja katika Msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) unalipwa kama uliyesali zaidi ya miaka miwili na miezi katika misikiti ya hapa nyumbani”, alisema.

 

Sala moja kuisali Makka unalipwa kama uliyesali sala laki moja katika misikiti mengine usipokuwa Msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Msikiti wa Baytul Maqdis. Yaani kusali sala moja Makka unalipwa kama uliyesali zaidi ya miaka mia mbili na sabini katika misikiti ya hapa nyumbani”.

 

Sheikh Mohammed akasherehesha zaidi kwa kusema “Lau kama mtu atakaa Makka kwa wiki mbili tu basi kila sala atakayoisali atalipwa kama aliyesali miaka elfu tatu, mia nane na thamanini na nane” Abdul aliruka na kusema: “SUBHAAN LLAH, TAKBRII kumbe fedha wanazolipia Mahujaji hazilingani kabisa na ujira wanaolipwa. Ewe Mola tuwafikishe na sisi kwenda kutekeleza ibada ya Hijja”. Wote waliitikia “aamiyn”. Mwalimu Waleed akaendelea kuwaambia familia yake yaliyokhutubiwa na Sheikh Mohammed.

 

“Ndugu Waislamu mmoja wetu atakapowafikishwa kwenda Makka asije kughafilika na kughururika kama alivofanya yule mmoja baada ya kurudi Makka akawa hasali tena, alipoulizwa akasema.

 

“Mie hapa nilipo nadai kwani nimekaa Makka wiki tatu na kila sala moja kwa laki moja ukifanya hesabu hapo nina sala za miaka zaidi ya elfu tano na mia nane, umri ambao siufikii kamwe.” Sheikh aliongeza kusema: “yeyote atakayehiji na atakaporudi akazama katika maasi ni dalili ya kuonesha ibada yake ya Hijja haijakubaliwa.

 

Ndugu Waislamu ili Hujaji apate fadhila hizo ni lazima ajuwe shuruti za Ibada ya Hijja, hukumu zake, matendo yake na ayatekeleze ipasavyo, pia ajiweke mbali na yote yanayokatazwa na kuharamishwa akiwa ndani ya Ibada ya Hijja”.

 

Sheikh Mohammed akamalizia khutba yake kwa kusema: “thawabu na fadhila za Hijja hakuna anayezijuwa isipokuwa Mwenyezi Mungu tu peke yake , na watu hawazijuwi isipokuwa chache mno”. Akaifunga khutaba kwa dua. Mwalimu Waleed akaiambia familia yake: “baada ya kuyasikia hayo ndio nikasema ikiwa hizi ni miongoni mwa chache mno ya fadhila za Hijja, KWA NINI NISIHIJI MWAKA HUU?