Hakuna sababu ya kusubiria mpaka upate kinuamgongo chako ndio uhiji hali ya kuwa Umri na uwezo wa kisiha umeshakupita. Kwa nini huna uwezo wa kifedha kwa ajili ya kutekeleza Nguzo ya tano ya Kiislamu ambayo inayomlazimu kila Muislamu mwenye uwezo kuitekeleza, Jibu lako ni Mfuko wa Hijja.

Mwandishi wa Makala hii amelenga kutaka kuifahamisha jamii ya kiislamu juu ya dhana nzima ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Hijja na namna utakavyoweza kufanya kazi zake pindipo taratibu zitakapomaliza.

Ama kwa hakika Uanzishwaji wa Mfuko huu, utakuwa ni faraja kwa Wananchi wenye kipato cha chini na kipato cha kati kwa vile makundi hayo ya watu hawamiliki fedha za mkupuo mmoja kwenda kutekeleza ibada hiyo.

Mfuko huu utakuwa unakusanya michango ili kufanya uwekezaji na kutoa faida inayopatikana kutokana na uwekezaji huo kwa wanachama kwa lengo la kuwawezesha kutekeleza ibada ya hija.

Pia michango hio itajikita zaidi pindi itakapotokea majanga katika safari ambapo fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kuwafidia wanachama katika hali yoyote ya maafa ili kuwarahisishia huduma bila ya kutumia fedha zao.

Utafiti unaonyesha kuwa, Mataifa ya nje ya kiislamu yakiwemo Malaysia na Indonesia wamepiga hatua kubwa kupitia mfuko huu. Kwa namna moja ama nyengine wamekuwa wakipeleka idadi kubwa ya Mahujaji kwa mwaka.

Ukilinganinsha na sisi Tanzania ambapo takriban hupeleka mahujaji wasiozidi elfu 3000 kati ya idadi iliyotengwa ya 25,000. Aidha maandalizi yetu mara nyingi yamekuwa dhaifu na yanayokwaza utoaji wa huduma bora katika Hijja.

Pamoja na kuwa maandalizi ni dhaifu lakini pia mahujaji wetu wengi ni wenye umri mkubwa na wanaotegemea vinua mgongo kwa ajili ya kutekeleza ibada hii kwa vile hali zao za kiuchumi ni ngumu na kupelekea kushindwa kutekeleza ibada hii katika umri wa Ujana.

Vile vile watu wamekuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba nyumbani au katika vikundi vya Hijja ambapo uwekaji huo si rasmi na unakuwa hauleti tija kubwa kwa muwekaji, wala Taifa na ndio ikaonekana kuna haja ya kuanzishwa Mfuko wa Hija Zanzibar.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana imeona ipo haja ya kuhakikisha na wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wananufaika.

Uwepo wa fursa  ya  kuchangia kiasi cha fedha kidogokidogo mpaka kufika hatua ya kwenda kutekeleza ibada hiyo kupitia Mfuko wa Hijja uliopo kisheria utasaidia mengi.

Aidha Michango hiyo ya wanachama itajikita katika gharama za usajili, mafunzo, upimaji wa afya na chanjo, huduma za usafiri, Visa, passport, mahitaji wakati wa kusafiri, mapokezi, usafiri wa ndani, makaazi, chakula, uongozaji katika ibada, huduma za afya za kawaida, maelekezo, ushauri na operesheni za kurudi nyumbani hadi kutoka uwanja wa ndege.

Wanachama wa mfuko wa hija watakuwa wanatekeleza ibada ya hija kupitia Kampuni za hija za Zanzibar (vikundi vya hija).

Hata hivyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana haikukurupuka tuu juu ya hilo, imefanya utafiti wa kina kuona ni kwa namna gani  Watu wameridhishwa na kuanzishwa kwa mfuko huo.

Takriban utafiti umefanyika kupitia  baadhi ya maeneo mengi  ya nchi yetu, ambapo asilimia 70 wameunga mkono suala hili ambapo utekelezwaji wake ni Ibada.

Kwa kuwa kila mikakati inayoekwa au kupangwa  haswa ya kiserikali  lazima iundiwe Sheria, na Sheria ya nambari 2 ya mwaka 2007  ya Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana kifungu cha (55)(1) imeipa uwezo kuwa ni chombo pekee kilichopewa dhamana ya kusimamia huduma za Hijja Zanzibar.

Kwa mantiki hiyo uanzishwaji wa mfuko huo utaanza kupitia tangazo la kiserikali na utakuwa chini kamisheni ya Wakfu,  mfano wa mfuko huu ni kutoka nchi ya Meldev.

Kwa kuwa, Idara ya Hijja itakuwa ipo chini ya muundo wa Kamisheni ya Wakfu na Idara ya Hiija ndio unaoufanyia kazi Mfuko wa hija ni vyema kwa Wananchi kutambua kazi za Mfuko wa Hija ni kama zifuatazo:

KAZI ZA MFUKO WA HIJA

Kuratibu shughuli za Mfuko wa Hijja, Kuhamasisha wananchi kujiunga na kuchangia katika Mfuko wa Hijja, Kupokea fedha za michango ya wanachama na kuzihifadhi vizuri.

Kazi nyengine ni pamoja na kuziwekeza fedha katika biashara na vitega uchumi, kusimamia ugawaji wa mafao kwa wanachama wa Mfuko, kuandaa ripoti na kutunza kumbukumbu za Mfuko wa Hijja.

Aidha kazi nyengine za mfuko huo ni kuandaa na kusimamia Mipango na Mikakati ya uendeshaji na uendelezaji wa Mfuko wa Hijja.

UENDESHAJI WA MFUKO WA HIJA

Mfuko huu haujaweka vikwazo katika kujiunga, mtu yeyote anafaa kujiandikisha au kuandikishwa iwapo ana lengo la kutekeleza ibada ya hija kwa kupitia njia hii ya kudunduliza kutakuwa na aina tatu za wanachama.

Kwanza ni Mwanachama binafsi: (Personal Member) ambae atajaza fomu ya usajili yeye mwenyewe na akajilipia mwenyewe kutoka katika mshahara wake, pato lake au biashara zake kwa lengo la kutimiza ibada ya Hijja yeye mwenyewe au kumhijia mtu mwengine.

Pili ni Mwanachama mwenza ambae atalipiwa na mtu mwengine aliemsajili kuwa mwanachama kama ni baba, mtoto, mke, mume na hata mfadhili kwa lengo la kutimiza Hijja, huku fedha ya uchangiaji hutoka upande  mmoja  na hijja kufanywa na mtu mwengine.

Tatu ni Mwanachama kikundi, huyu atajumuisha watu wawili (2) na wasiozidi kumi (10) ambao wameweka nia ya kwenda hijja kwa kupokezana wenyewe kwa wenyewe kwa kuchangiana wenyewe kwa wenyewe.

Wanachama hawa huchangia kama kikundi na pesa zao zinaweza kumsafirisha mwanakikundi mmoja au watakaotosheleza kutokana na pesa zilizochangwa kwa muda ule, na wale wengine itawalazimu kusubiri michango ya miaka mengine.

Wana kikundi wenyewe ndio wanaopanga na kuamua namna bora ya kutekeleza hijja na Mfuko wa Hijja utasimamia kama mshauri, usimamizi na utekelezaji huo

Kila mtu ana njia zake za kupatia kipato na hilo limezingatiwa katika Mfuko wa Hijja. Kutakuwa na wachangiaji wa aina tatu kwa kuzingatia aina za kazi anayoitegemea katika kuwasilisha michango yake.

Mchangiaji Mwajiriwa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) atakuwa akichangia kwa njia ya kukatwa moja kwa moja sehemu ya mshahara wake na makato yake kuwasilishwa moja kwa moja kupitia akaunti ya kibenki.

Mchangiaji Mwajiriwa wa taasisi zisizo za Kiserikali, ambae pia atakuwa akichangia kwa njia ya kukatwa moja kwa moja sehemu ya mshahara wake na makato yake kuwasilishwa moja kwa moja kupitia akaunti ya Mfuko huo.

Mchangiaji Binafsi, ambae aliejiajiri mwenyewe au hajajiriwa katika sekta rasmi, mwanachama huyu anaweza kuchangia kupitia katika ofisi za Mfuko, Wakala wa Mfuko au amri kutoka Benki ya kukatwa katika Akaunti yake.

Mfuko unalenga watu wote hivyo umeweka kiwango cha chini cha kuchangia ni wastani wa $dola 20 za Marekani sawa na shilingii 46,000 kwa kuanzia.

Kiwango hiki kitamuwezesha mchangiaji kutekeleza Hijja ndani ya kipindi cha miaka 20 au kama utaona muda ni mkubwa unaweza kuongeza kima chengine unachoona mchangiaji kinafaa.

Hata hivyo wazo la kuweka kima cha chini zaidi ili kuwawezesha hata watoto kumudu kujichangia litawekwa katika sheria

Kwa vile lengo kuu la Mfuko huu ni kutekeleza ibada ya Hijja wanachama wa Mfuko utafikia kikomo cha kuwa mwanachama baada ya kukamilisha mchango na kupatiwa fao la Hijja.

Vile vile, Mwanachama mwenyewe anaweza kurejeshewa fedha za mchango au sehemu ya fedha pindi itakapojitokeza dharura za kisharia kama kufariki au kuritadi na mfuko ukaridhia kumrejeshea sehemu ya fedha au fedha zake zote

Mwanachama atatakiwa kuweka wasia iwapo atafariki na fedha zake zikitosheleza kumhijia aidha kumpeleka Hija mtu au kutumia viongozi wa Hija aweze kuhijiwa badala ya mchango wake huo kurithiwa na jamaa zake.

Hii ina maana kuwa haitoshi kuwa wewe ni mwanachama halafu usiweke wasia unapokuwa Mwanachama ni lazima uweke wasia mapema endapo utafariki fedha zako zitumike kwa kwenda kuhijiwa.

Bila shaka Mfuko huu, utakuwa ni chachu ya kuleta mabadiliko ya utekelezaji wa ibada ya hijja.

Tunaamini kuwa itapelekea watu wengi zaidi watekeleze ibada ya Hijja kwa wepesi na usahihi. Pia utatoa fursa kwa taasisi zinazoandaa safari za Hijja kufanya maandalizi mazuri na ya mapema.

Sio hayo tu Mfuko wa Hijja utachangia katika uchumi wa Nchi kwa vile fedha zitakazokusanywa zinaweza kuwekezwa katika shughuli mbali mbali za kimaendeleo na hatimae kuleta tija na maslahi kwa wanamfuko, wawekezaji na taifa kwa ujumla.

Tunamuomba Mola Mtukufu, Mola wa Mbingu na Ardhi na vilivyomo ndani yake ausimamishe Mfuko huu wenye nia njema kwa waislamu na awalipe malipo mema wale wote watakaochangia katika kuusimamisha na kuuendeleza.Amiin .

Wabilah Taufik