MAKAA ya mawe ni aina ya mwamba mashapo au mwamba metamofia na fueli kisukuu muhimu, inayotokea kutokana na mabaki ya mimea ya kale iliyogeuzwa kuwa aina ya mwamba katika mchakato wa mamilioni ya miaka.Kikemia ni hasa kaboni, Kijiolojia inatokea kama kanda pana au nyembamba katikati ya miamba mengine.

Huchimbwa mara nyingi katika migodi chini ya ardhi au kama iko karibu na uso wa ardhi katika machimbo ya wazi yaliyo kama mashimo makubwa.

Takwimu zinaonesha kuwa makaa ya mawe yanachangia asilimia 41 ya umeme unaozalishwa duniani, umeme wa maji asilimia 16, umeme wa gesi asilia asilimia 20, nyuklia asilimia 15 na umeme wa mafuta kwa kutumia jenereta ni asilimia sita tu kutokana na kuwa umeme ghali.

Utafiti umebaini kwamba miongoni mwa mataifa yaliyoendelea kiuchumi duniani ni yale ambayo yanatumia umeme wa makaa ya mawe.

Mataifa hayo ni pamoja na Afrika Kusini inayotumia asilimia 93 ya umeme wa makaa ya mawe, Poland asilimia 92 na China asilimia 79.

Nchi nyingine ni Australia asilimia 77, Kazakhstan asilimia 70, India asilimia 69, Israel asilimia 63, Jamhuri ya Czech asilimia 60, Morocco asilimia 55, Ugiriki asilimia 52, Marekani asilimia 49 na Ujerumani asilimia 46.

Tanzania katika kutekeleza Dira ya Taifa ya mwaka 2025 inatarajia kuzalisha umeme wa makaa ya mawe ambayo yameenea katika mikoa ya kusini, hususan mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Iringa na Njombe.

Hii inatokana na Sera Taifa ya Madini ya mwaka 1997, inasisitiza juu ya sekta binafsi kuendeleza madini ambapo serikali katika sera hiyo ina jukumu la kuidhibiti, kuikuza na kuiendeleza sekta hiyo.

Meneja Shirika la Bandari Mtwara, Noubat Kalembwe, amesema kwamba, walianza usafirishaji wa makaa hayo ya mawe mwezi Novemba 2021, na mpaka sasa wamesafirisha tani 305,692.3 kukiwa na meli sita zilioifanya kazi hiyo.

Alisema usafirishaji huo ulianza Mwezi Novemba, na kufuatiwa Januari, Machi, na Aprili meli mbili zilisafirisha rasilimali hiyo huku mwezi wa Mei ni Meli moja tu ilisafirisha mzigo huo wa makaa ya mawe.

Kalembwe aliongeza kuwa shehena hizo za makaa ya mawe ya Tanzania, zilielekezwa katika masoko ya nchini India, Egpty, Senegal na meli ya mwisho iliielekea nchini Uholanzi.

“Usafirisahji huo umekuwa ukifanywa na kampuni ya Ruvuma, inayotumia eneo hilo takribia skwea mita 25,  na kwa kila meli wamekuwa wakichukua mzigo huo kwa siku 30 na baada ya hapo huita meli lakini Bandari kwa ajili ya kuupakia hutumia siku tano wa mzigo 60,000.

MATARAJIO

Meneja huyo alisema katika kuifanya kazi hiyo vizuri zaidi,  wanategemea kuwa wasafirishaji zaidi, kwani tayari kuna maombi waliyoyapokea ya wanaotaka kusafirisha makaa ya mawe.

Akiyataja Makampuni hayo, ni STAMIKO na makampuni mengine manane, Kujitegemea, jambo ambalo hivi sasa limewafanya kuvuka malengo ya makusanyo katika Bandari hiyo kwa takribani asilimia 36.

Alisema katika kuifanya kazi hiyo walijiwekea malengo ya kuhudumia tani 377, 700 lakini mpaka sasa wameshahudumia tani 520,000.

Aliongeza kuwa mahitaji ya makaa ya mawe hivi sasa yamekuwa makubwa jambo ambalo linaifanya Bandari hiyo kutoa huduma kubwa kwa siku ambazo meli za kupakia kutia nanga katika bandari ya Mtwara, kwani tayari kuna mataifa yanataka kununua bidhaa hiyo ikiwemo Uturuky.

Sambamba na hilo, alisema kwa siku wamekuwa wakipokea magari 70 hadi 80 ya makaa ya mawe yanayotaka kusafirishwa kupitia Bandari hiyo, na huweza kukusanya tani 2001 hadi 2004 na mzigo unapokamilika ndio hupakiwa kwa kuondoshwa kwenda katika masoko ya ndani nan je ya nchi.

Alisema meli inayotarajiwa kusafirisha makaa hayo ilitarajiwa kufika Juni 9, mwaka huu ambayo itapakia makaa ya mawe makubwa na nyengine Juni 25, 2022.

Kalembwe aliongeza kuwa kazi hizo wanazozifanya wamekuwa wakizingatia suala zima la uhifadhi wa mazingira, kwani katika usafirishaji wa makaa hayo hutawaliwa na vumbi, jambo ambalo hudhibitiwa na mifereji ya maji iliyowekwa katika eneo hilo ili kuwe na usafirishaji salama.

CHANGAMOTO ZINAZOWAPATA

Kalembwe anasema moja ya changamoto inayowapata katika bandari hiyo ni sehemu ya kuyahifadhi ambayo hivi sasa wanaendelea kuyatafuta maeneo   mapya, kwani hapo awali walipanga kuwepo kwa kampuni tatu lakini sasa zimeongezeka.

WAWEKEZAJI WATOA NENO KWA RAIS SAMIA

Mtendaji wa kampuni ya Ruvuma Coal Ltd, Ryan Weinard, alisema wanampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuwafungulia milango ya kusafirisha makaa ya mawe jambo ambalo limewafanya kurahisisha kuipata bidhaa hiyo Tanzania.

Alisema wanafarijika kufanya kazi zao katika Bandari hiyo kutokana na kuungwa mkono katika ufanyaji wa kazi zao kwa wakati wote wanaposafirisha  bidhaa yao kiasi ambacho wanaoiona Tanzania iko vizuri katika uwekezaji kwa vile wanapata ushiriikiano mkubwa katika operesheni zao zote wanazozifanya.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, alifanya ziara ya kuangalia hali halisi ya utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi katika kuitekeleza sera hiyo.

Akiwa katika Bandari ya Mkoa wa Mtwara, Katibu Shaka aliishuhudia utekelezaji wa sera hiyo, kwa kujionea kwa macho yake juu ya utekelezaji wa ilani ya CCM, alisema kumekuwa na mzigo mkubwa unaosafirishwa katika mataifa ya nje.

“Leo hii, tayari kuna meli za mataifa ya nje zimekuwa haziadimiki katika Bandari hiyo ya Mtwara kubeba mali ghafi hiyo ya makaa ya mawe kiasi ambacho Shaka ameridhishwa na kazi inayofanyika katika eneo hilo”, alisema.

Shaka alisema hivi sasa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imeamua kutenga fedha za kuiimarisha Bandari hiyo ambayo hivi sasa inatia tija kwa taifa kwa bidhaa hiyo ya mkaa wa mawe.

Aliongeza kuwa Rais Samia hakuna jambo kubwa alilolifanya la kuwainua watanzania kiuchumi, na mradi huo wa usafirishaji wa makaa ya mawe utakuwa chachu ya kuiongezea mapato serikali.

Alisema uuzaji wa makaa hayo inatokana na Rais Samia kuifungua diplomasia ya nchi hii na ameiongoza Tanzania kama tayari ameshakaa miaka mitatu madarakani jambo ambalo limeifanya nchi kurudi katika ramani ya dunia.

Tanzania hivi sasa ni kinara wa diplomasia ya kiuchumi, jambo ambalo limechangia kukiheshimisha Chama cha Mapinduzi katika mageuzi ya kiuchumi.

Alisema hiyo ni kutokana na Mkoa huo wa Mtwara kuanza kufunguka kiuchumi kutokana na miradi mbali mbali ya kimkakati inayotekelezwa na serikali hivi sasa.

“Mimi nilipokuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana mara yangu ya mwisho kuja Mtwara haikuwa hivi, nilioiacha miaka hiyo sio hii ya leo imebadilika sana, kuna miundombinu ya barabara, fursa za kiuchumi, fursa za kiuekezaji zimekuwa kwa kiwango kikubwa kuna maingiliano ya kibiashara, hivi sasa nimeshuhudia Wakenya wapo hapa, Uganda na nchi nyengine za jirani wanakuja kuchukua bidhaa sasa anazuka mtu mmoja anasema Mama hatumuelewi nani kasema” alisema Shaka.

Alisema watanzania wanapaswa kukataa propaganda zinazotolewa na baadhi ya watu hao za kutaka kufifirisha maendeleo ya Tanzania kwani wanaye Rais anaejuwa watu wake wanataka nini na anaeumwa na changamoto za watanzania.

“Ilani ya uchaguzi ya CCM inasema ndani ya miaka mitano kwa wabunge wote wapiganie maendeleo yaliopo katika utekelezaji wa ilani na sio matakwa yao binafsi ila ni kwa ajili ya serikali na wananchi”, alisema Shaka.

Alisema ni muhimu jamii kutumia makaa ya mawe kuzalishia umeme kwa sababu gharama zake ni nafuu kwa wananchi na pia umeme huo utachochea ukuaji wa viwanda nchini.

Shaka aliongeza kuwa katika kuimarisha huduma katika bandari hiyo mamlaka ihakikishe upatikanaji wa makasha (Makontena), pamoja na  kununuliwa kwa mitambo ya kupakia na kushusha mizigo na tozo bandarini kupitiwa ili kuipa bandari hii ufanisi na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa mkoa huu na kuwa neema kwa wananchi.

Licha ya madini ya makaa ya mawe kulalamikiwa kuchafua mazingira duniani kote, utafiti umebaini kuwa umeme unaotokana na madini hayo ndio unaotegemewa zaidi na mataifa mengi yaliyoendelea duniani.

Madini hayo ya makaa ya mawe ambayo yanachimbwa Tanzania kwenye Mgodi wa Ngaka, wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma yanaongoza kwa ubora duniani na kabla ya kuanza rasmi mgodi huo, taarifa zinaonesha kwamba zaidi ya tani 1,000 za makaa ya mawe zilisafirishwa kupelekwa nchini Afrika ya Kusini. ili kuchunguza ubora wa madini hayo.

Matokeo ya utafiti huo alisema uliofanyika kuanzia mwaka 2008 umeonesha kuwa ubora wa madini hayo haufanani na madini ya makaa ya mawe yanayochimbwa katika nchi yoyote duniani.

Katika Utafiti huo, umebaini kuwa mgodi huo unakadiriwa kuwa na zaidi ya tani milioni 400 za makaa ya mawe hivyo Watanzania aliwataka kuthamini uwepo wa madini hayo na kuwapongeza TPA na wawekezaji wanaojishughulisha na kazi ya kusafirisha makaa hayo ambayo ni hazina kwa taifa.