MPIRA wa magongo ni miongoni mwa michezo mizuri ambayo miaka ya nyuma iliwahi kutamba na kuiletea sifa nzuri Zanzibar ndani na nje ya nchi.
Sambamba na hilo pia wapo wachezaji ambao enzi zao waliwika kwa kuwa na kiwango kizuri cha mchezo ambapo waliitangaza vyema Zanzibar baada ya kuibuka washindi katika mashindano mbalimbali.
Lakini jambo la kusikitisha hivi sasa ni kuwa mchezo huo katika miaka mingi unaonekana kupoteza muelekeo katika dira ya Zanzibar, jambo ambalo linasikitisha kuona mchezo uliongíara kwa kipindi kirefu unapoteza haiba yake machini mwa mashabiki.
Bila ya shaka pengine zipo sababu kadhaa ambazo zimesababisha kutokea kwa hali hiyo, lakini, kwa ujumla mchezo wa mpira wa magongo haupo vizuri kwa sasa.
Mbali na changamoto ambazo zinaweza kutajwa katika hili, lakini moja jambo moja kubwa linalochangia kuwepo na hali hii, ni pamoja na ukosefu wa kiwanja cha kuchezea.
Kiwanja kimekuwa ni miongoni mwa changomoto inayowakabili wachezaji wa mpira wa magongo hivi sasa.
Suala la uwanja ni hatua moja kubwa ambayo kama haitafanyiwa kazi kwa haraka, mchezo huu unaweza kuendelea kudidimia kila siku zinavyoendea kwani hakuna mchezo ambao unaweza kuchezwa kwa ustadi wake bila ya kuwepo kiwanja kizuri.
Hivi sasa wachezaji wa mchezo huu wamekuwa wakihangaika kutafuta uwanja wa kufanyia mazoezi, kwani hapo awali walikuwa katika uwanja wa Mao Zedong kabla ya kufanyiwa matengenezo makubwa.
Lakini, baada ya kukamilika matengenezo hayo, wanamichezo wa mpira wa magongo hawakurejeshwa na hivyo kuwafanya kuhangakia sehemu za kufanyia mazoezi.
Kama kweli kuna nia ya dhati ya kutoka kurejesha mchezo huu katika ramani yake, ni vyema kwa serikali kupitia mamlaka husika kuhakikisha wanalitafakari kwa kina na kulitafutia ufumbuzi mzuri.
Kama hili litashindwa kutekelezwa kama kwa ufanisi mzuri na unaotakiwa, Zanzibar itaendelea kupoteza hadhi yake katika michezo ambayo ina uwezo mkubwa wa kuitangza na kuongeza idadi ya watalii.
Lakini jambo jingine ambalo si zuri hata kidogo katika mchezo huu, ni pale unapowaona wachezaji wengi wanaocheza mchezo huu ni kutoka vikosi vya ulinzi, huku raia wa kawaida wakiwa habari yoyote juu ya mchezo huu.
Changamoto nyengine ni kuona vijana wa Zanzibar wapo nyuma kabisa kushiriki mchezo huu, kulinganisha na wazee ambao ndio wanaonekana viwanjani kwa wingi.
Suala la vifaa nalo pia ni jambo jengine ambalo linaweza likawa kikwazo kikubwa katika kufikia mafanikio kupitia mchezo huo, kwani hivi sasa baadhi ya wachezaji wanafanya mazoezi bila ya vifaa vizuri.
Mbali na baadhi ya changamoto hizo, bado tunaamini ipo nafasi nzuri ya kulirekebisha hili na tukaweza kupata mafanikio, endapo tutaweka mikakati maalum ya kuukwamua mchezo huu.
Ili kuhakikisha mchezo huo unarejesha hadhi yake, viongozi husika wanapashwa kufanyakazi ya ziada ya kuupeleka mchezo huu maskulini kwa ajili ya kutafuta wachezaji vijana.