SERIKALI imesitisha ushuru wote wa mahindi yanayoingizwa nchini kwa nia ya kuimarisha usalama wa chakula.

Hatua hiyo itakuwa afueni kwa Wakenya huku bei ya unga ikitarajiwa kushuka.

Kwa sasa bei ya pakiti ya kilo 2 ya unga wa mahindi inauzwa shilingi 210 za Kenya kutoka shilingi 140 mwezi uliopita.

Katibu wa Baraza la Mawaziri la Kilimo Peter Munya alisema kukomeshwa kwa ushuru unaotozwa uagizaji wa mahindi kutahakikisha kuna upatikanaji wa mahindi ya kutosha nchini na hivyo kupunguza gharama ya uzalishaji wa unga.

Akizungumza katika mpaka wa Namanga Jumanne baada ya kukutana na washikadau kadhaa kushughulikia tatizo la uhaba wa mahindi, Munya alisema mahindi yote yanayoingizwa nchini kutoka Tanzania na mataifa mengine ya COMESA yatasamehewa kutozwa ushuru.