WAUMINI wa dini ya kiislamu wa Zanzibar waliokusudia kufanya ibada ya Hija tayari wameanza kuwasili huko Makka nchini Saudi Arabia kutekeleza ibada hiyo ya faradhi kwa waislamu wenye uwezo.

Baada ya kukosa ibada hiyo takriban miaka miwili kufuatia kuibuka kwa ugonjwa wa Corona duniani, tayari mahujaji kutoka nchi mbalimbali wameanza kuwasili Saudia baada yugonjwa huo kupungua sana duniani.

Kwa hapa Zanzibar kundi la kwanza la mahujaji limeanza kuwasili hapo juzi, ambapo, jana na leo pia makundi mengine yametarajiwa kuwasili huko Makka kwa ajili ya ibada hiyo kongwe katika historia ya uislamu.

Kama ilivyotajwa katika Quran tukufu, kwamba wako waliofika kwa usafiri wa ndege, wanyama, gari nakadhalika kutegemea na ukaribu au matakwa ya wahusika waliokusudia kutekeleza ibada hiyo.

Kwa kuwa ibada ya hija ni falsafa ya kimwili, Ibada hii inalenga kuwakumbusha Waislamu historia ya harakati za Kiislamu zilizoanzia Mjini Makka na kufikia kilele chake cha mafanikio Mjini Madina.

Ni ibada inayoamsha ari ya kujitoa kwa hali na mali kwa ajili ya dini ya Mwenyezi Mungu. Ni safari ndefu ya gharama ambayo inaakisi utayari wa kujitoa kwa ajili ya dini ya Mwenyezi Mungu.

Hija ni zoezi la kimwili linalotokana na imani ya Hujaji kwamba hakuna chochote chenye thamani katika dunia hii kama utii kwa Muumba. Mithili ya askari waliojumuika pamoja baada ya kutii amri ya Kiongozi, mkusanyiko wa Mahujaji Maka ni ishara ya utii kwa Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, swallallahu alayhi wa sallam.

Ni mkusanyiko wa aina yake unaotimiza dhana ya Umma mmoja bila kujali tofauti za rangi, kipato, elimu, jinsia na kadhalika. Kama kila Hujaji atahiji kwa mazingatio basi inaweza kujengeka nidhamu ya hali ya juu baada ya Ibada hiyo ambapo kila mtu atabadili maisha yake na kuishi kwa utii kama alivyoonesha utii katika hatua zote za ibada hiyo.

Matendo yote ya kiroho na matendo yote ya kimwili katika ibada ya Hija yanalenga kuuandaa Umma wa Waumini Duniani kwa mapinduzi ya kiroho na kimwili ili ulimwengu uhame kutoka maisha ya kutenganisha mwili na roho ambayo yameleta janga kubwa la kimaadili na kijamii duniani kote.

Kuiacha roho pekee yake bila mwili hakutimizi hitajio la UchaMungu kwani utawa pekee hauwezi kuijenga dunia. Na kuuacha mwili pekee bila roho hakutimizi hitajio la kimaadili ambalo ndilo linalouchunga mwili katika kila nukta ya maisha.

Kwa kuizingatia Ibada ya Hijja, kila Hujaji atakuwa amejenga maisha ya uwiano wa roho na mwili katika kuzikabili changamoto za maisha ya dunia kwa ufanisi. Ibada ya hija inaakisi kisimamo cha Siku ya Kiama ambacho kitakuwa cha kiroho na kimwili.

Kwa sababu hiyo, maisha ya roho na mwili ya kila mwanadamu lazima yasalimishwe kwa Mfalme wa Siku ya Mwisho kama yanavyosalimishwa katika ibada ya Hija.

Hivyo tunaamini kuwa mahujaji wetu wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla watatekeleza ibada hiyo kwa usalama na amani na kurudi nyumbani salama.

Ni wazi kuwa mara baada ya waislamu kurudi kutekeleza ibada hiyo watayatekeleza kwa vitendo yale yote waliyoyafanya huko Makka Saudia Arabia.

Tujaalie na sisi ambao hatijapata nafasi hiyo kwa njia moja ama nyengine atuwezeshe kufanya ibada hiyo kabla ya kutuhitaji kwake. Amiin.