KWA miezi kadhaa sasa waumini wa dini ya kiislamu hapa Zanzibar wamo kwenye matayarisho ya kuelekea nchini Saudi Arabia katika miji mitukufu ya Makka na Madina kwenda kutekeleza ibada ya hijja.
Ibada hiyo ni nguzo ya tano, kati ya nguzo zinazojenga na kuisimamisha dini ya kiislamu, ibada ambayo hufanywa kwa wakati mahususi, kwenye maeneo mahususi na masharti mahususi.
Janga la ugonjwa wa corona lililoukumba ulimwengu, limesababisha miaka miwili iliyopo Saudi Arabia kuzuia kupokea mahojaji, hata hivyo kidogo hali imerejea baada ya kupungua kwa maambukizi ya ugonjwa huo duniani kote.
Kwa mujibu wa taarifa mwaka huu, mahojaji 2,700 kutoka Tanzania baadhi yao tayari wameshafika nchini Saudi Arabia na wengine wako njiani kuelekea nchini humo tayari kwa ajili ya kutekeleza ibada hiyo ambayo ni nguzo ya tano katika dini ya kiislam.
Kwanza kabisa tunawaombea kheri mahujaji wetu waliokwisha anza safari na wale waliomo kwenye matayarisho ya mwisho tayari kwenda kuitikia wito wa Mwenyezi Mungu.
Aidha kwa moyo mkunjufu kabisa tunapenda kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awape afya na siha njema ili waitekeleze vyema ibada hiyo kama inavyotakiwa.
Hata hivyo, tunapenda kuwaasa sana mahujaji wetu wapya na waumini wa kiislamu kwa ujumla, watofautishe kwenye akili zao, baina ya ibada ya hijja na kwenda Makka.
Kwa tunavyo fahamu, kwenda hijja ni kuweka nia ya dhati na kutekeleza kwa mitendo yanayo juzu kufanywa kwenye ibada hiyo kwa mujibu wa mashatri, nguzo na sunna za ibada hiyo.
Kwa hiyo unapotaka kwenda hijja maana yake ni kwamba, lazima uhakikishe na uzingatie kila kitu kinakwenda kama kilivyoamrishwa katika kuitekeleza ibada hiyo.
Kwenda Makka na Madina ni tofauti kidogo na kwenda hijja, kwani kwenda Makka na Madina ni kufuata mkumbo kufanya ibada hiyo bila ya imani thabiti, kuwa istiizai moyoni, kwenda kwa sababu watu wamekwenda na hata kufanya ria.
Kwa hivyo, mtu anakwenda Makka hana tofauti na yule anayekwenda kufanya utalii kwa kushangaa magorofa ya mji, uzuri wa misikiti, miundombinu iliyokamalika na miji iliyopangwa vizuri, hivyo haina tofauti na kutembea Mji Mkongwe.
Kuna taarifa nyingi tunazipata zinazotofautisha baina ya kwenda hijja na kwenda Makka, wakati mwengine tunasikia wengine hupotea tangu siku ya kwanza na huonekana siku ya mwisho watu wakiwa wameshamaliza ibada.
Hata hawajijui wala hawajitambui wanafanya nini kwa sababu hiyo ibada yenyewe hawakuiwekea nia thabiti, watu wa namna hii wamekwenda Makka hawakwenda hijja kwa sababu Makka na mji hijja ni ibada.
Aidha mtu aliyekwenda hijja pia huonekana baada ya kurudi, tunaweza kumtambua jinsi atakavyo jibidiisha katika kuilea hijja yake, sambamba na kuondokana na makandokando yote yenye kutia shaka dhidi ya imani ya kiislamu.
Lakini kwa waliokwenda Makka hata wakirudi hawabadiliki, kama walikuwa na roho dhaifu huendelea nayo, kama watu wa mujungu ndio huzidi, kama msengenyaji ataendelea, kama mchawi ndio hakamatiki, kama wazinifu ndio hubeba hadi vitoto anavyoweza kuvijukuu.
Tungependa sana kuwaona mahujaji wetu wanatekeleza hijja na sio kwenda Makka, huku tukiwaombea Mwenyezi Mungu awaongoze kwa afya njema na usahihi wa matendo ya ibada yenyewe.
Mahujaji wetu pia watumie fursa hiyo kwenye ziara ya maeneo matakatifu kuiombea amani nchi yetu, tuepuka mifarakano na hitilafu ndogo ndogo ambazo zinaweza kutugawa.
Pia wawaombee wana jamii waondokane na maradhi ya nafsi kama vile, chuki, hasada, ushikina, uchawi, choyo, ubinafasi, dhulma mambo ambayo yamekuwa yakiufidisi umma wa kiislamu kwa wakati huu.