MAENDELEO ya teknolojia katika mawasiliano yamefikia hatua kubwa na yamekuwa na faida sana, ambapo kuna tofauti kubwa miaka 30 iliyopita na hali ilivyo katika maisha ya hivi sasa.

Nakumbuka enzi za zamani kidogo, kama familia imepata msiba na maiti yuko hospitali ya Mnazi Mmoja, hutafutwa kijana shababi anayeweza kusukuma vizuri baiskeli na kupeleka taarifa za kifo umbali wa kilomita 40.

Baada kijana kufika na kutoa taarifa maandalizi ya mazishi huanza na kijiji chote hupokea taarifa hiyo, hata hivyo kutokana na maendeleo ya tekolojia leo mambo hayo hayapo.

Hivi sasa unaweza kutumia simu yako na kuandika ujumbe mmoja na utawafika zaidi ya watu bilioni moja katika muda wa sekunde chache, bila ya hata kuinua mguu wa kwenda kuisambaza taarifa uliyonayo.

Hapa ndipo ninapoweza kusema na ndio tafsiri maendeleo ya teknolojia ya habari yameufanya ulimwengu wa kisasa kuwa kama kijiji.

Pamoja na faida kubwa za matumizi ya mawasiliano, kinacho nisikitisha ni kwamba hivi sasa matumizi ya vifaa hivyo vya mawasiliano zikiwemo simu na kompyuta za mikononi, yamezidi mno kiasi cha watu kuwa kama watumwa.

Kuna vijana wengi katika familia zetu hawalali usiku kucha wanachati na kuzungumza, mambo ambayo hayana maana na ni kuhatarisha afya zao.

Kuna baadhi ya watu hawezi kupitisha siku bila ya kuingia kwenye mitandao ya simu, na kwamba bahati mbaya sana sio kama anaingia kuna mambo ya maana, bali anaangalia na kusoma na kuangalia mambo yasio na maana wala faida

Nakubali kwenye mitandao kumeundwa magurupu mazuri ambapo watu hupata nafasi ya kujadili mambo mbalimbali yanayohusua maisha, lakini yapo magurupu ya yanayorushiana habari za ufuska, yapo magurupu yanayopanga njama ovu, yapo magurupu ya umbea nakadhalika.

Kwa ufupi hayo ndio maisha ya watu wengi katika jamii ya kizazi cha sasa, ambapo inafikia hatua mtu yupo tayari asile wala asilale, lakini ahakikishe anapata simu ya ‘android’ ili afaidi raha za mitandao.

Kinachonisikitisha sana ni kuona katika baadhi ya ofisi watendaji wanapoteza muda mwingi wakiwa kwenye mitandao akitoa fecebook, whatsup, Instagram, twitter, youtube mtu mmoja ana mitanado si chini ya mitano na yote yupo ‘online’ tena yupo ofisini.

Tusishangae kuona ofisi nyingi zinashindwa kufikia matarajio ya kiutendaji kwa sababu wafanyakazi hawawajibiki vizuri kutokana na muda mrefu kuwa kwenye mitanado ya kijamii.

Tafiri nyingi zilizofanywa katika miaka ya karibuni zinaonesha kuwa matumizi ya muda mrefu kwenye mitandao ya kijamii imeanza kuwatia watu maradhi ya aina mbalimbali.

Si vibaya kuwa na mitando ya kijamii, lakini kila mwanajamii ahakikishe inatekeleza vyema wajibu wake na pia tuitumie kwa kujifunza mambo mazuri tusiyoyajua na sio mambo maovu.