UMOJA wa Afrika (AU) umetuma waangalizi kufuatilia Uchaguzi Mkuu unaotegemewa kufanyika Agosti mwaka huu nchini Kenya.

Kwa mujibu wa taarifa iliotolewa na Umoja huo inaeleza kuwa timu ya wachunguzi wa kimataifa na kitaifa wanategemewa kuwasili nchini humo.

“Kufuatia mwaliko wa Serikali ya Jamhuri ya Kenya kwa Umoja wa Afrika kuangalia Uchaguzi Mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Agosti 9, 2022, Tume ya Umoja wa Afrika inatuma ujumbe wa wataalamu wa kimataifa wa uchaguzi nchini Kenya unaojumuisha wataalam wa timu nane,” ilisema. taarifa ya AU iliotolewa tarehe 27 Juni.

Timu hizo zinapaswa kutathmini maandalizi ya uchaguzi wa Kenya, mienendo ya kisiasa na usawa wa kampeni za uchaguzi.

Aidha AU ilieleza kuwa, timu kuu itakuwa na kazi ya kufuatilia maandalizi ya uchaguzi, kutathmini mienendo ya kisiasa na ushindani wa kweli na usawa wa kampeni ya uchaguzi, pamoja na kudumisha mawasiliano ya mara kwa mara na wadau wa kitaifa na kimataifa kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Pamoja na hayo pia itatuma timu nyingine ya waangalizi wiki chache kwenye uchaguzi, na baadaye waangalizi wengine wengi wa muda mfupi wiki moja kabla ya siku ya uchaguzi.

Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki mapema mwezi Mei lilituma ujumbe wa pamoja wa tathmini ya kabla ya uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi usio na ghasia, haki na wa kuaminika ambao utaimarisha mchakato wa kidemokrasia nchini Kenya.