TEHRAN, IRAN

MAOFISA  wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa wameelezea wasiwasi juu ya ukiukwaji wa haki za binaadamu nchini Iran, katikati ya ripoti za kuongezeka kwa visa vya watu kunyongwa, ikiwa ni pamoja na watoto na wahamiaji kutoka Afghanistan, wanaotuhumiwa kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya.

Maofisa hao walisema hayo wakati ripoti ya mwaka kuhusu Iran iliyoandikwa na katibu mkuu Antonio Guterres ilipokuwa ikiwasilishwa kwenye baraza la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa.

Ripoti hiyo imekusanya taarifa kutoka taasisi za serikali zilizoonyesha watu 310 walinyongwa mwaka 2021, tofauti na 260 mwaka 2020.

Hata hivyo balozi wa Iran kwenye Umoja wa Mataifa ameliambia baraza hilo kwamba madai hayo ni ya uwongo na hayana msingi.