HIVI karibuni taifa la Tanzania litafanya zoezi muhimu kwa maendeleo yaani sensa ya watu na makaazi kwa mujibu wa sheria maalum ya takwimu sura 351 kifungu kidogo cha 6(2)(a) na hufanyika chini ya usimamizi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS).

Sensa ya watu na makaazi ni utaratibu mzima wa kukusanya, kuchakata, kuchambua na kusambaza taarifa za kidemografia, kiuchumi, kimazingira, umri, viwango vya elimu, hali ya vizazi na vifo katika jamii za watu wote na makaazi yao na taarifa nyengine nyingi katika nchi yoyote kwa kipindi maalum, kwa kila mtu aliyelala ndani nchi usiku wa kuamkia siku ya sensa.

Aidha sensa ya mwaka 2022 itakuwa ni sensa ya sita tokea kufanyika muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 na sensa ya kwanza ilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012 kwa mikoa 18 ambapo Tanzania bara ni mikoa 13 na Tanzania visiwani ni mikoa mitano.

Pia sensa ya mwaka 2022 itafanyika katika kipindi cha utekelezaji wa mpango mkakati wa umoja wa mataifa wa kufanya sensa kwa miaka ya 2020 ulioanza mwaka 2015 hadi 2024 (The 2020 United Nations Round Of Population And Housing Census) na Tanzania ni mmoja wa wanachama katika umoja huo.

Ni ukweli usiopingika kuwa sensa ya watu na makaazi hufanyika kwa lengo la kupata takwimu za msingi za watu na hali za makaazi ambazo zitasaidia kutunga sera, kupanga na kufuatilia mipango ya maendeleo ya kimkakati inayolenga kukuza ustawi wa nchi na watu wake.

Hata hivyo, matokeo ya sensa ya mwaka huu yatasaidia serikali na wadau wengine kufuatilia na kutathmini malengo yaliyofikiwa katika kutekeleza mipango ya maendeleo iliyokusudiwa kwa lengo la kukuza uchumi na kupunguza umasikini.

Sambamba na hilo, lakini semsa hiyo itatathmini utekelezaji wa mpango wa pili wa taifa wa maendeleo wa 2016/17 hadi 2020/21, mpango wa pili wa kukuza uchumi Zanzibar (MKUZA II), na kupima mpango wa tatu wa taifa wa maendeleo 2021/22 hadi 2025/26.

Aidha, kuweza kutathmini utekelezaji wa dira ya taifa ya maendeleo ya mwaka 2025, dira ya maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050 pamoja na kupanga takwimu za msingi za kufanya maandalizi ya dira nyingine ya taifa ambayo mchakato wake unaendelea ndani ya serikali.

Vilevile Serikali inahitaji kujua idadi ya watu katika kila familia na maeneo ya utawala ili kurahisishia juhudi za kupeleka na kuimarisha huduma muhimu za kijamii kama huduma za afya, maji safi na salama, shule, na hata miundo mbinu ikiwemo ya barabara.

Ambapo hata kwa upande wa kilimo na wafugaji sensa husaidia kujuwa idadi ya wakuli na wafugaji na mahitaji yanayohitajika kwa wakulima na wafugaji sahihi kamavile, mbolea, mbegu, madawa na hata madaktari wa mifugo na mabwana shamba.

Pia upangaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo serikali inahitaji kufanya kwa kuzingatia takwimu za watu zinazopatikana kutokana na sensa ya watu na makazi kuanzia ngazi ya shehia hadi taifa.

Katika utekelezaji wa zamira ya serikali ya kuendesha uchumi kwa njia ya kidigitali hivyo ni lazima kupatikane takwimu sahihi za watu, makazi yao pamoja na shughuli wanazazifanya.

Lakini ukusanyaji wa takwimu sahihi kwa kutumia teknolojia ya kisasa utarahisisha utekelezaji wa mipango ya serikali katika ukusanyaji wa mapato, kuwa na mifumo jumuishi ya kifedha, mifumo bora ya bima za afya pamoja na mifumo imara ya mawasiliano kwa njia za simu na mitandao.

Ikumbukwe katika ufunguzi wa nembo ya sensa rais wa zanzibar alisema kuwa tuzingatie kwamba idadi yetu ni mtaji wetu, tunapaswa tuijuwe ili tuitumie vizuri hivyo sensa ni zoezi muhimu ambalo kila mmoja kwa binafsi yake analazimika kushiriki na kutimiza wajibu wake ili kuhakikisha inakuwa ya mafanikio makubwa na kuendana na kauli mbiu inayosema ‘Sensa kwa maendeleo, jiandae kuhesabiwa’.

Sensa huongozwa na kamati maalumu kuanzia taifa hadi kitongoji/kijiji/mtaa ambapo ngazi ya taifa kuna kamati kuu ya sensa ya watu na makazi na huongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamo wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na maofisa wengine wa juu wa serikali walioteuliwa kufanikisha kazi hiyo.