BIASHARA huria ni suala lililotiliwa mkazo kwa kuwa kila mmoja aweze namna ya kujitafuta riziki ya halali.
Aidha serikali daima imekuwa ikisisitiza wafanyabiashara kulipa kodi kwa maslahi ya taifa, hivyo uhuru walipewa kamwe wasiutumie vibaya na kuzipindisha sheria.
Katika visiwa vya Zanzibar wananchi wake wameonekana kukubali kuitika wito wa kufanya biashara kwani wengi wao wamejiajiri kupitia biashara mbali mbali ambazo zinawapatia kipato cha kujikimu na maisha yao.
Hata hivyo, baadhi ya watu wamekuwa wakikiuka sheria na kufanya biashara zisizokubalika, maeneo yasiyokubalika jambo ambalo wakati mwengine wanapochukuliwa hatua za kisheria kuilaumu serikali.
Siku za hivi karibuni katika mji wa Zanzibar kumeibuka bishara mpya ya kuchenjisha chenji hasa katika vituo vya daladala jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Wateja wakubwa wa kuchenjisha chenji wanaonekana ni magari ya usafiri wa umma (daladala) ambapo huchenjisha chenji kwa wanaofanya biashara hiyo.
Biashara hiyo ambayo ilikua ikilalamikiwa na wananchi wengi wakiwemo madereva na tingo wa daladala lakini hata wananchi kwa ujumla.
Katika biashara hiyo ambayo mwananchi anapokwenda kutaka chenji kwa shilingi 1000 hukatwa shilingi 200 na kurudishiwa 800 jambo ambalo lilikua linawaathiri wananchi wengi.
Kilio hicho kimeonekana kuliliwa na wengi kwani biashara hiyo ilikua haiwapendezi kwa kuwa huwaumiza lakini hata kuitia doa Serikali na nchi kwa ujumla.
Baada ya kilio hicho kuliliwa na wengi, mnamo Juni 24 mwaka huu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Ofisi ya Rais Fedha na Mipango ikiwataka wananchi kusitisha biashara hiyo mara moja.
Kupitia taarifa hiyo Serikali ilitia mkazo kwa kusema hatua kali zitachukuliwa kwa mwananchi yoyote atakaegundulika kufanya biashara hiyo huku ikizitaka kamati za ulinzi na usalama za Mikoa yote ya Zanzibar kutoa mashirikiano katika kufanikisha zoezi hilo.
Hili ni jambo jema na wajibu wa wananchi kuipongeza Serikali kwa hatua kubwa iliyoifanywa ya kuzuia biashara hiyo kwani ilikua inaleta picha mbaya kwa nchi yetu.
Hatuna budi kuipongeza Serikali kwa hatua waliyoichukua ya kufuatilia na kuona kwamba wafanyaji hawaendi kinyume na matakwa ya serikali.
Ni vyema wafanyabishara wa chenji wakatii agizo la serikali ikiwa ni pamoja na kufuata taratibu na sheria zilizowekwa kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.
Tukumbuke kuwa mjenga nchi ni mwananchi na mvunja nchi ni mwananchi.