PAMOJA na jitihada kubwa zinzochukuliwa na serikali na wadau katika kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa watoto, bado wapo watu katika jamii wanaoendeleza vitendo hivyo.

Cha kusikitisha ni kwamba wapo hata wazazi na walezi, waalimu na sasa hata kumeibuka tuhuma dhidi ya watoa huduma wa afya, kutajwa kujihusisha kufanya vitendo hivyo.

Mwaka 2019, ulikuwa kisirani kwa baadhi ya watoto na wanawake, kufanyiwa ukatili na udhalilishaji na madaktari kisiwani Pemba.

Mfano Novemba 21, mwaka 2019, katika hospitali ya Chake chake, daktari wa kitengo cha ‘Ultrasound’, alishikiliwa na ZAECA kwa tuhuma za kuomba rushwa ya ngono kwa mama mjamzito, kama sharti la kumpa huduma.

 

Kesi hiyo baada ya uchunguzi na kuhojiwa, alifikishwa mahakamani, ingawa Januari 1, mwaka jana aliachiwa huru, kwa sababu mbali mbali zikiwemo ushahidi dhaifu.

Mnamo Disemba 18, mwaka 2019, TBC 1 iliripoti ofisa muuguzi msaidizi wa kituo cha afya Mamba mkoani Katavi kushikiliwa na Jeshi la Polisi, kwa tuhuma za kumbaka mjamzito, wakati alipokuwa akimsaidia kujifungua.

Aprili 21, tena mwaka huu wa 2022, daktari mwengine anaefanyakazi kituo cha afya Gombani wilaya ya Chake Chake Pemba, (jina linahifadhiwa) naye ameingia kwenye tuhuma kama hizo ambapo hivi sasa anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa kaskazini Pemba.

Nae, kama walivyokuwa kwa madkatari wengine, wasiotekeleza wajibu wao vyema, akituhumiwa kumtorosha na kisha kumbaka mtoto wa mwenye umri wa miaka 16.

Daktari huyo miaka 35, ni mkaazi wa Kangagani, wilaya ya Wete mkoani humo, ambapo anadaiwa alimchukua mtoto huyo kutoka kwa rafiki yake, kisha alimpeleka kwenye nyumba anayoishi eneo la Kangagani, akidai kuwa kuna dawa alizozikosa hospitali, anaweza kumpatia huko.

Mtoto anasema kuwa, Aprili 21 mwaka huu, alikwenda kituo cha afya Gombani, kwa ajili ya matibabu na baada ya kupatiwa huduma na daktari huyo, alimuomba nambari yake ya simu.

Ilipofika usiku, walikuwa wanawasiliana kupitia ujumbe mfupi (sms), kwa lengo la kwenda kuchukua dawa nyingine ambazo kwa mchana huo, alizikosa hospitalini hapo.

“Nilikwenda hospitali kutibiwa, ugonjwa mapele sehemu zangu za siri, lakini akaniambia mpaka aje daktari mwengine, kwa hiyo kesho (siku ya pili yake), atakuja kunichukua, ili ukanipe dawa nyingine”, anasimulia mtoto.

Siku ya pili wakati yupo skuli, daktari huyo alimpigia simu na kumeleza kuwa, akirudi skuli, amsubiri kwa rafiki yake, mpaka atakapotoka kazini daktari huyo, ili akamchukue kwa ajili ya kumpatia dawa nyingine.

‘’Alikuja kunichukua, nikijua anaenda kunipa dawa nyingine, kumbe alinipeleka hadi nyumbani kwake na kisha baada ya kunipima Ukimwi alinibaka,’’anasimulia.

‘’Usiwe na wasi wasi wowote wewe uko salama na mimi niko salama, hatuna maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, na kisha aliniletea futari na,’’anafafanua.

Mtoto huyo alidai kuwa, daktari huyo (mtuhumiwa) anapokwenda kazini, alikuwa anamfungia mlango, ingawa baa ya siku ya tano alimtoa na kuandoka eneo hilo.

Mama mzazi nae alidai kuwa, mwanawe aliondoka kwenda skuli, ingawa alikuja kupata wasiwasi kuona ilipofika saa 9:00 jioni, kuwa hajarudi na kuanza kupiga simu kwa ndugu na jamaa wa karibu.

Aliporudi mumewe (baba mzazi wa mtoto) akamueleza kuwa mtoto wao, hajarudi na ndipo walipochukua uamuzi wa kwenda kituo cha Polisi Chake Chake kutoa taarifa.

“Ilipofika siku ya tano nilimpigia simu nikampata, nikamtaka arudi, na alitii agizo hilo na alipofika nilimpeleka kituo cha Polisi Chake chake, ambapo awali walipeleka malalamiko,’’anasimulia.

ATHARI YA VITENDO

Vitendo hivyo dhidi ya watoto ni suala zito linalowanyima haki zao za kibinadamu ambalo humkosesha haki zake za msingi ikiwemo kuishi, kupata elimu na afya bora.

Watoto wanapofanyiwa vitendo vya udhalilishaji ikiwemo ukatili na unyanyasaji hushindwa kufurahia utoto wao kwani kuwaletea madhara makubwa kiakili, kihisia na kimwili.

Hali hii isipokomeshwa ni wazi kuwavitendo hivyo vitaendelea kuongezeka na hata kusababisha umasikini katika jamii zetu.

Bila shaka kila mmoja amepitia hatuwa ya utotoni kama tafsiri ya mtoto inavoolekeza kuwa mtoto ni mtu yoyote mwenye umri chini ya miaka 18.

Tafsiri ambayo imetokana na mkataba wa kimataifa wa haki za watoto,mkataba wa afrika  kuhusu haki na ustawi wa mtoto pamoja na sharia ya Mtoto nambari 6 ya mwaka 2011 ya Zanzibar.

UTOAJI USHAHIDI

Suala la kutowa ushahidi limekuwa kikwazo kikubwa kwa jamii zetu na ndio maana wanaoshughulikia kesi hizo hupata mwanya wa kujificha na mwisho wa siku kufutwa kwa kesi hizo kwa ubwete kabisa.

Mkurugenzi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sharia wilaya ya Mkoani Nassor Hakim, alisema ni jukumu la jamii kufanya kila mbinu kuhakikisha wanafika mahakamani kutowa ushahidi.

“Waliowengine wanadhani hakimu na mwendesha mashataka, ndio wanaweza kumaliza kesi zote na msitakiwa kufungwa, wakati sio sahihi,’’anasema.

Mwanaharakati Omar Haji Omar alisema si vyema kuvunjika moyo kwa kikwazo chochote kwani kufanya hivyo ndio kutoa mwanya wa kuzizimishwa kesi hizo.

Mratibu wa wanawake na watoto Shehia ya Mchanga mdogo Siti Khatib Ali alisema lazima jamii iungane katika kutoa ushahidi.

Alisema wanaotenda matendo ya udhalilishaji wamekuwa wakifuatilia watu iwapo kama wanafika mahakamani kutoa ushahidi na kama wanachoka na wao hupata nguvu ya kuyaendeleza matendo hayo.

Sheha wa shehia ya Kiungoni Wilaya ya Wete Omar Khamis Othman, alisema ushahidi mahakamani ndio kigezo cha mtuhumiwa kutiwa hatiani.

Alisema katika shehia yake wanajipanga kuhakikisha wanasaidiana nauli ili kufika mahakamani kutowa ushahidi.

Afisa ustawi wa jamii wilaya ya Wete, Haroub Suleiman Hemed, alisema ni wajibu wa jamii katika kupambana na kutokomeza udhalilishaji wa kijinsia jambo ambalo kabla walidhani ni la kazi ya taasisi fulani tu.

Arafa Abdi wa Mkoani alisema ni vyema kukapitiwa vyema sheria ya ushahidi, kwani haimtendei haki mtoto aliyefanyiwa udhalilishaji kwa vile hutowa ushahidi kwa alilofanyiwa na mwisho wa siku kesi hufutwa.

“Tena maneno ya mara ya mwanzo ya mtoto aliyedhalilishwa ni bora yakarekodiwa kwani hakutokuwa na udanganyifu,”anasema.

WAATHIRIKA WA VITENDO VYA UDHALILISHAJI  

Baadhi ya watoto kuanzia miaka 5 hadi 17 ambao ni waathirika wa udhalilishaji, wanasema, elimu ya kujengewa ujasiri wa kutoa ushahidi mahakamani, imewasaidia.

Bado kundi la watoto linakumbana na kadhia inayofanywa na baadhi ya watendaji wa vyombo vya sheria kwa kuchukuwa rushwa ya pesa na vitu vya thamani kwa lengo la kupotosha ushahidi.

“Sisi kama waathirika wa vitendo vya udhalilishaji hasa wenye hali ngumu ya kimaisha, hiyo tabia imekuwa ni changamoto kubwa yenye kutupa wakati mgumu,’’anasema mmoja.

Watoto hao walivitaka vyombo vya sheria kufanya kazi kwa uadilifu ili haki itendeke kwa pande zote mbili, na kuondosha tatizo hilo katika visiwa vya unguja na Pemba.

Hata hivyo walliiomba seikali kuwa kesi za udhalilishaji zisiwe na mawakili kwani ndio kichaka kikubwa wanachotumia upande wa mtuhumiwa kwa wale wenye pesa zao na uwezo  fulani  wa kifedha ama madaraka fulani .

VYOMBO VYA SHERIA

Mwanasheria dhamana ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka Pemba Ali Haidar, asema hakuna mashitaka ambayo mtu anatiwa hatiani, bila ya kuwepo mashahidi.

“Sisi waendesha mashtaka hatufahamu lolote iwapo kuna kosa limefanyika vijijini, sasa kama wakija watu kutoa ushahiodi au kupinga juu ya tendo fulani ,sasa hapo ndio ukweli hupatikana,”alieleza.

Kwa upande wake Hakimu wa mahakama ya Mkoa Chakechake Luciano Makoye Nyengo alisema mashahidi wote wanaofika mahakamani wamekuwa wakipewa nauli zao kama kawaida.

Alisema kukosekana kwa nauli hiyo kusiwarejeshe nyumbani mashahidi, maana suala la kutowa ushahidi ni haki yao, hasa katika kuusaidia muhimili wa mahakama, kufanikisha kazi zake.

“Jamii ijipange vyema kuhakikisha wanakuwa na hamu kufika mahakamani kutowa ushahidi, kwani hakuna kesi ambayo itafikia tamati pasi na kuwepo kwa mashahidi,” alisema.