ONGEZEKO la hivi karibuni la ghasia na vita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limesababisha wimbi jipya la wakimbizi kuvuka na kuingia nchi jirani ya Uganda, na hivyo kuongeza hatari ya eneo hilo kukabiliwa na wimbi jipya la Covid-19.

Zaidi ya wakimbizi 62,000 wa Kongo wameingia Uganda tangu Januari na idadi hiyo imeongezeka katika wiki chache zilizopita kufuatia mapigano mapya kati ya vikosi vya serikali na waasi wa M23.

Kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu la Uganda, wengi wa wakimbizi hao hawajachanjwa dhidi ya Covid-19.

Itifaki ya shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu kuhudumia wakimbizi ni kwamba wakimbizi wanapaswa kufanyiwa uchunguzi wa kiafya kuhusu magonjwa kadhaa, ikiwa ni pamoja na Covid-19, katika vituo vya kuwapokea karibu na mpaka.

Hata hivyo imekuwa vigumu kwa serikali ya Uganda  kudhibiti mienendo ya wale wanaotoka DRC, huku wengi wao wakikataa kwenda kwenye vituo rasmi vya mapokezi kwa ajili ya kuchunguzwa, wakiamua kubaki mpakani wakisubiri mapigano kupungua.

Msemaji wa Shirika la Msalaba Mwekundu la Uganda Irene Nakasiita ameliambia gazeti la The East African kuwa, “Kwa hofu ya kushughulikiwa kama wakimbizi, wengi waliweka makazi ya muda katika mpaka ambapo wanachanganyikana na jamii,”

Kufikia Alhamisi, data rasmi ilionyesha kuwa Uganda ilikuwa imetoa dozi milioni 21.7 za chanjo ya Covid-19, kati ya hizo milioni 16 zilikuwa dozi moja na dozi milioni 10 mara mbili.

Nchi hiyo ina lengo la kuchanja takriban watu milioni 21.9, ambao ni asilimia 49 ya watu wote ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Na ingawa hakuna data rasmi kuhusu ni kesi ngapi za Covid-19 zimegunduliwa kati ya wakimbizi, maafisa wa afya wa Uganda bado wana wasiwasi kuwa wakimbizi wanaweza kuhatarisha afya.

Kufikia Jumatano, kulikuwa na wastani wa kila siku kesi 98 mpya  za Covid-19 zilizogunduliwa nchini Uganda na wakuu wa afya nchini humo wanatabiri kuwa kutakuwa na maambukizo mapya zaidi ya 1,000 mwishoni mwa wiki hii.

Kesi za Covid-19 zimekuwa zikiongezeka Afrika Mashariki, huku kampeni za serikali za chanjo zikipungua sambamba na watu wengi kupinga chanjo.