MICHUANO ya Soka ya Wanawake ya Chalenji Afrika Mashariki na Kati, tayari yameanza kutimua vumbi nchini Uganda, ikiyashirikisha mataifa manane ya ukanda huu.
Mataifa hayo ni wenyeji Uganda, Burundi, Djibouti, Ethiopia, Sudan Kusini, Tanzania Bara, Rwanda na Zanzibar.
Tunachukuwa nafasi hii kuitakia kila heri timu yetu ya Zanzibar Queens pamoja na dada zao wa Kilimanjaro Queens ambao kwa pamoja wanabeba jina la Tanzania kupitia Muungano wetu.
Michuano hiyo inayosimamiwa na Baraza la Vyama vya Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), imerejea baada ya kukwama kutokana na janga la ‘corona’ lililokuwa limeikumba dunia kwa miaka kadhaa.
Zanzibar ambayo ni miongoni mwa waanzilishi wa CECAFA, imekuwa mshiriki wa uhakika wa michuano hiyo kwa karibu kila mwaka, licha ya kukabiliwa na changamoto kadhaa katika uendeshaji wa soka la wanawake nchini.
Kwa bahati mbaya, akinadada wetu hawajakuwa na matokeo mazuri kwenye michuano hiyo katika miaka ya nyuma ambapo imekuwa ikipoteza mechi zote za hatua ya makundi.
Pamoja na kutofanya vizuri, lakini, wawakilishi wetu hao wamekuwa wakionesha utofauti fulani wa kiwango ikilinganishwa na miaka inavyosonga mbele na kuleta matumaini fulani kuelekea mafanikio siku zijazo.
Kubwa linaloonekana kwa akinadada wetu ni kukosa uzoefu sambamba na maandalizi duni kutokana na timu hiyo kuandaliwa bila ya kuwepo mikakati bora kuelekea michuano hiyo.
Hali hiyo inapelekea wachezaji hao kutokuwa na ubora wa ushindani kulingana na namna ya uzoefu wao wa kucheza mpira wa miguu, tofauti na mataifa mengine kama Tanzania Bara, Kenya, Uganda na Burundi ambayo kwenye siku za karibuni zimekuwa na ligi bora ya soka ya wanawake.
Kutokana na hali hiyo, tunaamini umefika wakati sasa wa kuweka nguvu katika ligi ya soka ya wanawake huku ikizingatiwa mahitaji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na lile la Afrika (Caf), la kuwepo kwa maendeleo ya soka ya wanawake kwenye mataifa wanachama.
Tunachokiamini ni kuwa Zanzibar imejaaliwa kuwa na vipaji vingi vya michezo na kinachohitajika ni kuwepo kwa mikakati iliyoandaliwa vizuri ili itoe taswira bora ya kisoka iliyopo nchini ambayo tayari imejengewa muundo mzuri kuanzia soka ya vijana kwa madaraja tofauti.
Lakini, pia tunaamini kama Zanzibar ambayo haina ushiriki mwengine wa peke yake kwenye mashindano kama ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ama lile la dunia (Fifa), michuano ya Chalenji ni fursa pekee inayopaswa kutumiwa kuwatangaza wachezaji wetu nje ya mipaka yetu.
Tunachokiamini ni kuwa akinadada wetu wanaouwezo na kinachohitajika ni mipango na utayari kwa vyombo vyetu vinavyosimamia michezo katika kuinua soka ya wanawake na michezo mengine kwa ujumla.
Changamoto ni sehemu ya kuelekea mafanikio na hayo tuliyokutana nayo kwenye michuano ya miaka ya nyuma iwe sehemu ya kupambana kwa ajili ya maendeleo ya baadae.
Tuendelee kuiunga mkono Zanzibar Queens kwa ajili ya maendeleo na hatma bora ya ya soka ya wanawake nchini.