SANAA ya muziki ni moja ya fani maarufu duniani kote iliojizolea mashabiki wengi kutokana na burudani yake inayopatikana.

Umaarufu huo hutokana kwa njia mbali mbali ikiwemo kutunga mashairi, mipangilio ya muziki pamoja na uimbaji ambao huwafanya mashabiki kupata burudani wanayoipenda.

Lakini mbali na hilo umuhimu wa fani ya sanaa ya muziki husaidia katika wasanii wenyewe, kujiajiri lakini pia kufikia malengo yao ikiwemo kuwa maarufu wao binafsi na nchi zao.

Tumeshuhudia  kuona wasanii wengi kushiriki katika matamasha mbali mbali duniani, ambayo huwasaidia katika kuonesha kazi zao na wengi wao kuzikubali.

Hili ni jambo jema kwani faida nyingi hupatikana ikiwemo ajira ya kuweza kutatua changamoto zinazowakabili, ambayo ndio jambo la msingi katika maisha ya sasa hivi .

Kwa hapa visiwani kwetu sanaa ya muziki nayo haipo nyuma kwani tangu miaka na miaka, tumeshuhudia ikifanya vyema katika kufikisha ujumbe kwa jamii.

Kadiri siku zinavyokwenda fani hiyo inaonekana kuzidi kuchanja mbunga kwani kila kizazi kinachozaliwa nacho hujikita katika fani hiyo.

Hivi karibuni katika visiwa vya Zanzibar tumeshuhudia vikundi viwili vya muziki vikiondoka nchini na kwenda Barani Ulaya kwa ajili ya kutoa burudani.

Vikundi hivyo ni pamoja na kile cha Siti & the Band pamoja na kikundi cha taarab asilia cha wanawake kinachojulikana kwa jina la Tausi Women Taarab .

Vikundi hivyo ambavyo vikiwa katika nchi hizo vitatoa burudani mbali mbali, zenye asili ya muziki wa taarab na Zanzibar kwa ujumla.

Lakini mbali na hilo wasanii hao katika ziara zao hizo wataweza kutoa mafunzo mbali mbali, ikiwemo historia ya muziki wa taarab na ngoma nyengine hapa Zanzibar pamoja na historia ya utamaduni wa Zanzibar.

Kutokana na hayo yote wasanii ni jambo la kufahamu kwamba ziara wanazokwenda, katika nchi za Ulaya na kwengineko duniani ziwe na tija ya kuitangaza vyema nchi yetu.

Kufanya hivyo kutaleta mafanikio mengi nchini ikiwemo kuisaidia Serikali yetu katika kuitangaza vyema nchi katika sekta mbali mbali mbali ikiwemo utamaduni na utalii.

Lakini mbali na hilo tu kazi watakazozifanya zitaweza kuwaleta watalii wengi kuja kuitembelea Zanzibar na kujifunza mambo mbali mbali .

Ni wajibu wa wasanii wetu mliondoka nchini na kuelekea nje ya nchi kuhakikisha ziara zenu zinaleta tija kwenu na taifa kwa ujumla.

Ni fursa pekee kwa wasanii wetu kuitangaza vyema Zanzibar ili tupate umaarufu kitaifa na kimataifa na mafanikio mengi ambayo yataijenga Zanzibar kuwa kituo kikubwa cha maswala ya utamaduni.

Huu ni wajibu wetu sote kwani kupata nafasi ya kufanya kazi ya sanaa katika mataifa makubwa ni kuitumikia nchi na kuonyesha uzalendo wa hali ya juu katika kuitafutia mafanikio.

Waswahili wanasema ‘mjenga nchi ni mwananchi na mbomoa nchi ni mwananchi’ ,hivyo wasanii wetu tuichukue kauli za mjenga nchi ili mtuletee mafanikio mengi katika kazi yenu hiyo.