WATOTO ni hazina muhimu kwa maisha kila siku. Hazina hiyo kamwe haitoweza kuwa muhimu endapo haitoandaliwa vizuri sambamba, kulindwa na kupewa hifadhi dhidi pingamizi zozote zinazoweza kuiangamiza.

Tunasema hivyo kwa sababu tunanasibisha maneno hayo na maneno ya hekima ya wazee wetu ambao waliamini samaki mkunje angali mbichi au udongo upate ulimaji.

Si samaki wala udongo ila ni maandalizi ya watoto au jambo lolote lile ambalo ungependa likupatie manufaa katika maisha yako linahitaji kufanyiwa maandalizi mazuri.

Maandalizi haya yatokane na jamii ambayo inaheshimu watoto kwa kuwatimizia haki zao kwa ajili ya kuwa na kizazi bora katika jamii.

 

Lakini hali hiyo haiwezi kufikiwa kama jamii itakosa mwelekeo wa kuuona umuhimu wa kwanza kujiendeleza wao wenyewe na kisha kufahamu umuhimu wa elimu kwa ajili ya kuwakumbusha watoto wao.

 

Kila siku zinavyokwenda hali habari zinazochapishwa katika vyombo vya habari juu ya maswahibu yanayowapata watoto, kusema kweli hazipendezi na hazionekani kwamba hazina hiyo iko kwenye hifadhi bora.

 

Moja ya tatizo linalowakabili watoto ni kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji ikiwemo kubakwa, kulawiti na hata kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kutisha kabisa.

 

Udhalilishaji na ukatili kwa watoto limekuwa janga kubwa hapa Zanzibar na kwamba kumeshawekwa mikakati kadhaa, lakini bado wimbi la vitendo hivyo linaongezeka.

 

Ukiachana na hilo kuna tatizo la kubwa ajira za watoto, ambapo wazee kwa kusingizio cha kuwafunza mwenendo wa maisha huwabebesha majukumu mazito yasiolingana na uwezo wao.

 

Ajira hizo zinafanywa na watoto hao wakiwa chini ya umri na wakiwa hawana hata maarifa ilhali wanapaswa kuufaidi utoto wao kwa kupata fursa ya kucheza na wenzao, lakini pia kwenda skuli na kushiriki kikamilifu kusoma.

 

Inaonesha kuwa mazingira kama haya wanayolelewa watoto hawa yatawakosesha kufikiri kuwa elimu na mambo mengine ya msingi ya mtoto ni stahili yake.

 

Kwa kuzingatia athari za kutowasimamia watoto kwenda skuli kunaweza kuzaa familia zitakazoshindwa kwenda sambamba na mbadilikoya teknolojia ya kisasa.

 

Na hata akitokea mmoja ama wawili wamefanya vyema na wanahitaji mchango wa kuwapeleka mbele zaidi ni wazi kuwa kizazi kama hicho kitashindwa kutimiza ndoto za hao waliofunuka macho kwa kuelewa kuwa elimu ni ufunguo wa maisha.

 

Iwapo watoto hawana mtu wa kuwakumbusha kuachana na biashara kama hizo na badala yake wasome inawezekana na wao pia wakashindwa kukumbuka umuhimu huo.

 

Inashangaza kuona bado tunaendekeza ajira za watoto wakati Jumuiya mbalimbali za kitaifa na kimataifa na hata za watu binafsi zimekuwa zikikemea na kutoa mbinu muafaka kwa ajili ya jamii kujitafutia kipato badala ya kuwaaachia watoto wao.

 

Tutegemee nini miaka 15 ijayo iwapo kumekuwa na ongezeko la watoto wanaojishughulisha na ajira zinazoweza kuwaletea madhara zaidi ikilinganishwa na faida?

 

Hakuna asiyefahamu kuwa kuna umasikini, lakini umasikini huo ni njia ya kufikiri namna gani jamii inaweza kukikinga kizazi kijacho dhidi ya ufukara kwa kutafuta mbinu halali na salama za kujitafutia riziki.

 

Kama watoto wanavyohitaji kushirikishwa katika masuala yanayowahusu ni fursa hiyo hiyo kuwapa uelewa kuhusiana na athari za umasikini sambamba na mbinu za kupambana nao.

 

Inawezekana kupambana na ajira za watoto kwa lengo la kuwa na kizazi bora kilichobobea taaluma mbali mbali kwa kuanza kuwapeleka skuli kwanza.