SEKTA ya utalii ni sekta muhimu sana ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa kwa uchumi wa Zanzibar.

Sekta hiyo ni miongoni mwa rasilimali muhimu sana hapa Zanzibar kwani inayochangia ukuaji wa uchumi na pato la taifa kwa asilimia zaidi ya 27 kupitia watalii  wanaotembelea Zanzibar kutoka nchi mbalimbali.

Pamoja na mambo mengine lakini utalii wa visiwa vya Zanzibar huchangiwa kwa kiasi kikubwa kuweko kwa fukwe mwanana, majengo ya kihistoria hasa ya mji mkongwe, magofu, ulimaji wa viungo (spice) na mengineyo.

Serikali ya awamu ya nane chini ya uongozi wa Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa kutambua kwamba utalii ndio rasilimali muhimu ya pato la taifa inaendelea kuimarisha sekta hiyo hasa kupitia mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini (MKUZA) sambamba na malengo ya milenia na dira ya 2030.

Hata hivyo, kufuatia mchango wa utalii, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, haikusita kuimarisha miundombinu mbalimbali ya utalii ikiwemo mawasiliano, usafirishaji, ulinzi na usalama, ujenzi wa hoteli za kisasa na upatikanaji wa elimu kwa ngazi na fani zote kupitia vyuo vya ndani na nje ya nchi.

Pamoja na serikali kufanikisha kwa kiasi kikubwa kuweka miundombinu inayowezesha kuleta ustawi na tija kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika sekta ya utalii lakini wapo baadhi ya watu wanaiharibu sekta hiyo.

Tumeshuhudia hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari vikiripoti juu ya kuwepo kwa watu wanaojiita “mabeach boy” wanaotembeza watalii.

Watu hao wamekuwa wakichukua watalii na kupotosha historia ya Zanzibar sambamba na kuwauzia vitu ambavyo vinakwenda kinyume na maadili, silka, utamaduni wa Zanzibar ikiwemo dawa za kulevya.

Katika siku za hivi karibuni kumezuka mtindo kwa baadhi ya watu hasa hao wanaotembeza watalii (wasiorasmi) yaani wasiosajiliwa ambao hukimbilia mashamba hasa sehemu za hoteli kubwa za kitalii kufanya wanavyotaka bila ya kujali kuwa wanaharibu na kuchafua sekta hiyo kwa kuwaonesha mambo mabaya watalii ambao wengine wana heshima zao.

Ni vyema wakafahamu kuwa kufanya hivyo kutashusha lengo la serikali la kupata watalii wengi hapa Zanzibar na kushusha pato la taifa kupitia sekta hiyo, pato ambalo linategemewa katika kuendesha maendeleo mbalimbali ikiwemo afya, miundombinu ya barabara, elimu nishati, huduma ya maji safi na salama na maendeleo mengine.

Miaka ya nyuma tulikuwa tukishuhudia matukio mbalimbali ambayo yalikuwa yakiwapata watalii ikiwemo kupigwa na kunyanganywa vitu vyao jambo ambalo lilikuwa likiitia doa sekta hiyo na Zanzibar kwa ujumla katika uso wa dunia.

Hatuna budi kuipongeza serikali kwa kuweka mazingira mazuri kwa wageni wanaoitembelea Zanzibar ikiwemo CCTV ambapo kwa kiasi kikubwa matukio hayo yameondoka kabisa hapa nchini.

Sasa umefika wakati kuona jambo hilo linasimamiwa kwa nguvu zote na serikali kupitia kamisheni iliyopewa jukumu la kusimamia suala la utalii nchini, kwa kuanzisha zoezi la kuwakamata watu hao na kuwachukulia hatua stahiki ikiwemo kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.

Kufanya hivyo, kutakuwa ni fundisho kwao na watu wengine wenye tabia kama hiyo, kila mmoja atimize wajibu wake kwa nafasi aliyonayo, huku tukikumbuka kuwa mjenga nchi ni mwananchi.