‘’KIPINDI cha mvua wanafunzi hulazimika niwafungie wasije madrasani mpaka zitakapo malizika,’’ hayo ni maneno ya Sada Khamis Hamad mwenye ulemavu wa viungo ambae ni mwalimu wa madrssa.
Alisema ulemavu alionao si kikwazo kwake kwa kuwa anatimiza ndoto zake za kuwa mwalimu wa madrassa.
Hii ni baada ya kuukosa uwalimu wa skuli kutokana na changamoto za kadhaa ila hakukata tamaa kwa sababu hivi sasa ni mwalimu wa madrasa.
“Nilikuwa natamani siku moja niwe darasani nafundisha ila sikubahatika, sikusoma skuli hata darasa moja, kwani ilikuwa iko maeneo ya mbali na siwezi kutembea”, anakumbuka.
Alisema ukosefu wa kiti mwendo kwa wakati huo, na hasa kutokana na ukosefu wa fedha waliokuwa nao wazazi wake, ulimkosesha elimu ya skuli.
Yote hayo ni masikitiko ya Mwalimu wa Madrasa ya Qur-aan Sada Khamis Hamad mwenye ulemavu wa viungo anaeishi katika kijiji cha Shumba Vyamboni Wilaya ya Micheweni Pemba.
Ukhti Saada Khamis Hamad ambae ni mtoto wa sita katika familia yao, anasema suala la kukata tamaa na yeye lilikuwa mbali mno.
Baada ya miaka kadhaa, alishindwa hakuweza tena kwenda madrasa kutokana na hali yake na kwa vile hana usaidizi wa kigari ambacho chengemuwezesha kumsaidia.
Baada ya kuona anakosa kusoma, ndipo akamua anzishe madrasa yake mwenyewe baada ya kuhitimu kusoma Qur-aan ili kuiendeleza elimu yake.
“Nilisema ijapo kuwa sikuweza tena kwenda kusoma, lakini isiwe sababu ya kukaa tu nyumbani, ndipo nikamua nianzishe madrasa yangu, ili kuwafundisha watoto”, anaeleza.
Alisema huu ni mwaka wa nne tangu kuanzisha madrasa hiyo, ambapo alianza na wanafunzi wanne wawili wa kike na wawili wanaume na sasa ana wanafunzi 52.
CHANGAMOTO
Ukhti Saada alisema kuwa anakosa nayoiona na kumkosesha usingizi ni ukosefu wa sehemu salama ya kusomeshea wanafunzi kutokana na mazingira yake.
Kwake mazingira hayo, hayako sio rafiki, kwani kwa sasa anatumia kibaraza cha nyumba yao kuwafundishia wanafunzi wake.
“Nasumbuka sana hususan kipindi cha mvua barazani panakuwa hapasomeki inabidi wanafunzi wasije madarasa mpaka mvua zikate”, anasema.
Aisema kuwa wanafunzi wamekuwa wakikimbia na kwenda madrssa nyengine kwa kukosa sehemu salama za kufundishia.
“Si vyema nguvu zote zikaelekezwa kwenye ujenzi wa miskiti pekee, bali msingi wa dini ya kiislamu, ni uwepo wa madrassa za kisasa na sio kusomea barazani, hivyo nawaomba wale wote watakaogiswa na madrasa hii kutusaidia”, alisema.
WANAFUNZI WAKE
Asha Khamis na Ali Juma wanafunzi wanaosoma madrsa hiyo a ukhti Saada, wanasema hawaridhishwi na kitendo cha kusoma barazani.
“Kwakweli hatupendi kusoma mazingira haya, kwani pakiwa na jua hapakaliki, na kukiwa na mvua tunafungiwa kabisa,’’wanasema.
Wanasema kama kweli kuna nia ya dhati kwa wadau wa haki za watu wenye ulemavu na watoto kupata elimu, hakuna budi kuchangiwa na kujenga madrassa ya kisasa.
MAMA MZAZI
Hadia Salim Ameir, anasema Mungu amemjaalia kuzaa watoto wanne wote wenye ulemavu wa viungo ambapo mmoja alifariki.
“Nilikua nawazaa ni wazima lakini mwisho wake wanakua walemavu, na sikuwapeleka Hospital nikajua ni sababu gani ilopelekea hivyo”, anasema mama huyo.
Aidha alieleza kuwa anaishi katika mazingira magumu yeye na watoto wake kwani hata nyumba yao wanayoishi ni mbovu na haina hata huduma rafiki za vyoo kwa ajili yao.
“Baba yao ameshafariki huduma zote wananitegemea mimi na sina msaidizi, sina hata kazi ya uhakika ya kufanya maisha yangu ni magumu nahitaji msaada”, alieleza.
Alisema viongozi wa majimbo kama Mbunge au Mwakilishi hawajawahi kupita katika familia yao angalau kuangalia changamoto zinazowakabili.
Kwa upande wake Mratibu wa Baraza la Taifa la Watu wenye ulemavu Pemba, Mashavu Juma Mabrouk, anasema wamekua wakiwasaidia watu wenye ulemavu, ambao wanajishuhulisha na harakati mbali mbali.
Hata hivyo aliwashauri wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika madrassa hiyo, kuonesha mfano kwa kuanza kuchangishana fedha kwa ajili ya kuanzisha ujenzi wa madrassa ya kisasa.
“Sisi Baraza hatuna mfuko maalumu wa kumsaidia mtu mmoja moja kama huyo, kwani anayoyafanya ni mambo ya kijamii ispokuwa tunawaomba wanajamii kuchangia, ili aweze kujenga madrassa”, alishauri.
UONGOZI WA SHEHIA
Sheha wa shehiya ya Shumba vyamboni Time Said Omar, ameeleza kuwa mwalimu huyo anapata shida kwani anasomeshea wanafunzi wake katika baraza ya nyumba yao na wakati mwengine hukaa kwenye Muembe.
ALIsema ameshachukua jitihada mbali mbali kuhakikisha anapatiwa msaada wa kujengewa madrassa japo chumba kimoja, lakini bado hajafanikiwa.
“Nimeshawapeleka viongozi wengi ili kumsaidia lakini bado hatujafanikiwa na hivi sasa nimejipanga niende kwenye jumuia ya Milele Foundation kungalia uwezekano wa kusaidiwa”, alisema.
Sheha huyo alisema licha ya ulemavu wake lakini mungu amemjalia kipaji cha elimu ameshafika Dar-es-salamu kushiriki mashindano ya qur an, hivyo anahitaji kuungwa mkono kwa hali na mali ili kuendeleza kipaji chake hicho.
UONGOZI WA WILAYA
Nae Mkuu wa wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya, alisema anelewa changamoto ya mwalimu, huyo ingawa wanaangalia namna ya kumsaidia.
“Hakuna fungu maalum kwa ajili ya kumsaidia mtu mmoja mmoja kwa ajili ya kujengea nyumba ama Madrassa, lakini kama wakitokezea wahisani tutampekelekea”, anasema.
OFISI YA MUFTI
Msaidizi Katibu ofisi ya Mufti Sheikh Said Ahmad Mohamed, alisema ofisi hiyo ndio msimamizi mkuu wa madrasa zote za Qur-an, ahivyo, aliahidi kuonana naye.
“Nimevutiwa mno kuona kuna mwanamke tena mwenye ulemavu wa viungo ameanzisha mpango wa kuihuisha dini ya kiislamu, na sisi tutaangalia namna ya kumasaidia,” anasema.
KATIBA YA ZANZIBAR YA MWAKA 1984
Kifungu cha 10 (g) kinafafanua ‘kwamba serikali itawekea mazingira rafiki kwa makundi ya wagonjwa, waliojiajiri, wazee, watoto na watu wenye ulemavu’.
Aidha kifungu cha 12 (1) kimefafanua kuwa, ‘watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria’.’
SHERIA YA WATU WENYE ULEMAVU NO 9/2006
Kifungu cha 9, kinaelezea haki ya kupata elimu kwa watu wote wenye ulemavu na mafunzo mengine kama ilivyo kwa raia wengine.