ILI nchi yoyote duniani iweze kufikia malengo ya kimaendeleo, haina budi kuwa na mipango bora katika matumizi ya rasilimali zake, ili kuhakikisha zinakuwa endelevu na kuleta tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kwa kipindi kirefu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imekuwa ikilipigia kelele suala la usimamizi mzuri wa rasilimali zake za ardhi, kwa kuamini kuwa ndio chimbuko la maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kutokana na rasilimali hiyo, nchi inaweza kufikia hatua kubwa ya maendeleo kwa haraka, kupitia sekta mbali mbali, kama vile kilimo, uvuvi, mafuta na gesi asilia, pamoja na Uwekezaji katika sekta ya viwanda na biashara.
Lakini pia kutokana na ardhi, pia kuna rasilimali muhimu za mchanga na misitu au Hifadhi za Taifa, ambamo ndani yake, sekta ya utalii imejikita. ‘‘Kwa vyovyote vile ardhi ndio kila kitu’’, katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya binadamu.
Kwa kuzingatia dhana ya ardhi kuwa ndio rasilimali muhimu zaidi katika maisha ya kila siku ya binaadamu na ustawi wa Taifa letu, tulitegemea wale wote waliokabidhiwa jukumu la usimamizi wa rasilimali hii, wangekuwa makini, waadilifu na wanaojali dhima na dhamana walizokabidhiwa na Taifa.
Ni vyema ikakumbuka kuwa maendeleo ya kweli ya Wazanzibari, iwe yatokanayo na chakula, malazi au vyenginevyo, yatatokana na rasilimali nyeti ya ardhi.
Katika dunia ya leo, nchi kadhaa duniani zilizoendelea na zile zinazoendelea, zimeweka mazingatio na kutambua thamani ya kila robo ya hekta ya ardhi waliyonayo.
Kwa muktadha huo ni wazi kuwa kila eneo dogo la ardhi tayari limekewa mipango mizuri ya kuendelezwa, kutegemea na aina ya mradi au kazi iliyopangwa.
Kwa bahati mbaya hapa kwetu, pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali kama nilivyotangua kueleza, mambo yamekuwa kinyume chake.
Katika miaka ya hivi karibuni, kumeibuka uvamizi mkubwa wa maeneo ya ardhi za kilimo na kutumika kwa ajili ya shughuli za ujenzi wa makaazi ya kudumu.
Wengi wanaofanya vitendo hivyo, ni wale waliopata vibali rasmi kutoka mamlaka zinazosimamia ujenzi.
Ni jambo la kusikitisha na pengine kuogopesha sana kuona mamlaka hizo zinatoa vibali vya umiliki wa ardhi bila kuzingatia madhara yanayoweza kujitokeza hapo baadae.
Uvamizi huu wa ardhi za kilimo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya makaazi ya kudumu pia ukayahusisha maeneo ya ardhi yaliogaiwa eka tatu, ambapo Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Marehemu Abeid Amani Karume aliweka msisitizo kutumika kwa ajili ya kuendeleza kilimo pekee na si kwa matumizi mengine.
Maeneo mengi yaliokumbwa na kukithiri na kadhia hii yale ya wilaya ya Magharibi ‘A’ na ‘B’ pamoja na wilaya ya Kati Unguja.
Shehia za Kianga, Chuini, Mbuzini, Maungani, Jumbi, Tunguu, kijichi, Mbuzini, Mwera na nyingine nyingi, zimeathirika na uvamizi huo.
Ni dhahiri kuwa uvamizi huu umekuja kutokana na ongezeko la idadi ya watu wanaohamia katika wilaya hizo, sambamba na mahitaji ya makaazi.
Katika kuhakikisha suala la ardhi linakuwa chini ya usimamzi na matumizi bora, Serikali ilitunga sheria namba 8 ya mwaka 1994, ambapo chini ya usimamizi wa Kamisheni ya Ardhi Zanzibar inamtaka kila anaemiliki ardhi kuwa na hati za umiliki.
Aidha kutokana na sheria hiyo Serikali ikalazimika kuunda Kamisheni hiyo kwa minajili ya kuhakikisha ardhi ndogo iliopo inatumika vizuri, sambamba na kuondokana na migogoro iliyoshitaji nchini kwa kipindi kirefu.
Miongoni mwa majukumu ya kamisheni hii katika kufanikisha dhana ya kumiliki ardhi, ni kusimamia suala zima la upatikanaji wa hati miliki za kumiliki ardhi.
Vile vile kuzuia utoaji wa vibali kwa wananchi watakaobainika umiliki wao una mashaka au unakwenda kinyume na sheria za kamisheni hiyo.
Ni dhahiri kuwa Serikali ina nia safi na wananchi wake na ndio maana ikaanzisha Kamisheni hii kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo pamoja na kuwepo sheria hii pamoja na zile zinazosimamia taratibu za ujenzi, zilizokabidhiwa taasisi nyingine, ikiwemo halmashauri za wilaya, inashangaza wananchi wameendelea kujenga katika maeneo yasiostahiki.
Linaloshangaza na kusikitisha zaidi ni kuwa, wananchi wengi miongoni mwa wanaotumia maeneo hayo kwa shughuli za ujenzi, wana vibali kutoka taasisi zilizowekwa kisheria.
Kuwepo kwa jambo hili, kunafifisha lengo la serikali la kuwa na matumzii mazuri ya ardhi ndogo tulonayo.
Kwa mantiki hii, tunasisitiza na kuiomba serikali kufanya uhakiki kubaini watendaji wake wasio waaminifu waanoendesha uovu huu, kwa lengo la kujipatia maslahi binafsi, bila kujali ustawi wa Taifa na vizazi vijavyo.
Kutokana na umuhimu wa kulinda matumizi ya ardhi ni vyema kuweka mikakati madhubuti ya kulinda raslimali zetu nchini.
Kila mtu anawajibu wa kulinda rasilimali ya ardhi kuweka mustakibali mzuri wa matumizi ya ardhi.