MDAHALO kuhusu ushirikiano wa kilimo duniani: Mazao Kutoka Kenya na Soko la China, ulioandaliwa na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika Kuu la Utangazaji la China CMG, umefanyika Septemba kwa njia ya zoom.

Mdahalo huo, umewakutanisha wataalam wa kilimo wa China na wenzao wa Kenya, ambapo umefanyika katika ambayo China inaadhimisha “Tamasha la mavuno” kwa kalenda ya nchi hiyo.

Kwenye mdahalo huo wataalamu wa China na Kenya wamejadili fursa mbalimbali za ushirikiano kati ya pande hizo mbili kwenye sekta ya kilimo na hasa kuhusu uzoefu wa China katika kushughulikia usalama wa chakula.

Mdahalo huo umefanyika wakati shehena ya kwanza ya maparachichi kutoka Kenya ikiwa imeingia kwenye soko la China, ambapo msafirishaji wa maparachichi kutoka Kenya, Hasith Shah, alisema utaratibu wa karantini uliorahisishwa na mamlaka ya forodha ya China umeisaidia kampuni yake kuingiza maparachichi nchini China.

Mkurugenzi wa Idara ya maua na mboga ya Mamlaka ya kilimo cha chakula ya Kenya, Benjamin Tito, amesema kuwepo kwa sera bora za usafirishaji wa mazao ya kilimo nje ya nchi ndio msingi wa kukidhi mahitaji ya taratibu kali za forodha za China, na Kenya ikiendelea kuwa na sera imara, itaweza kuuzwa kwa bidhaa zaidi kwenye soko la China.

Katika mdahalo huo pia zimeoneshwa video za wakazi wa miji ya China wakizungumzia bidhaa za kilimo za Kenya zinazopatikana nchini China.

Mbali na maparachichi yaliyoingizwa nchini China kupitia bandari ya Shanghai, muuza matunda mmoja alisema anafahamu kuwa kutakuwa na bidhaa zaidi kutoka Kenya kwenye soko la China.

Profesa Fredah Rimberia amesema licha ya kuwa Kenya ina mazao mengi ya chakula, bado kuna safari ndefu ya kuona mazao mengine ya Kenya mbali na chai, kahawa na maparachichi yakiingia kwenye soko la China, sababu kubwa ni ubora.

Suala la ushirikiano kwenye mambo ya sayansi na teknolojia pia limejadiliwa kwenye mdahalo huo. Profesa Liu Gaoqiong wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Nanjing ambaye amekuwa akifanya kazi nchini Kenya kwa zaidi ya miaka 20 sasa, aona ushirikiano kwenye eneo la sayansi za kilimo ni moja ya njia bora, sio tu katika kuhakikisha mbegu bora zinapatikana, bali pia kuhakikisha usalama wa mazao.

Imefahamika kuwa changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi na kuongezeka kwa joto, sio kama tu imefanya uzalishaji wa mazao ya kilimo unaotegemea mvua ya asili kumepungua au hata kukwama katika baadhi ya maeneo, bali pia umefanya ukubwa, wingi na ubora wa mazao ya kilimo yanayozalishwa sasa kupungua.

Dk. Li Yuan ambaye ni mtaalamu wa lishe ya mimea, amesema kwa sasa kuna teknolojia nyingi zinazoweza kusaidia kukabiliana na tatizo la usalama wa chakula duniani.

Amesema teknolojia zilizopo zinaweza kufanikisha uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo katika eneo dogo na kuhakikisha usalama, lishe na ubora wa mazao hayo.

Alitolea mfano wa mboga za majani zinazotumia mjini Beijing, na kusema licha ya kuwa mji wa Beijing una idadi kubwa ya watu, mboga za majani zinazotumiwa na wakazi wa Beijing zinalimwa kwenye eneo dogo la mabanda (Greenhouse) ambako shughuli za kilimo zinafanyika kwa mwaka mzima bila kujali hali ya hewa.

Mdahalo huu umefanyika tarehe 23 Septemba ambayo ni siku ya “Tamasha la mavuno la China” kwa kalenda ya kilimo ya China. Siku hii ambayo mbali na kuashiria kuanza kwa msimu wa mavuno nchini China, pia inatumiwa na wachina kukumbuka juhudi mbalimbali zilizofanyika katika kuendeleza sekta ya kilimo nchini China.