RAIS Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amemaliza ziara yake ya siku 3 nchini China, baada ya kufanya mazungumzo na mwenzake wa China Xi Jinping na kufikia makubaliano kadhaa, na kusaini mikataba 15 ya utekelezaji wa hatua za ushirikiano.

Ziara hii imetajwa kuwa ni ziara yenye mafanikio makubwa, na imeweza kutimiza malengo mawili moja likiwa ni la kisiasa, na lingine likiwa ni la kiuchumi.

Kwa upande wa kisiasa, ziara hii imeweza kuondoa wasiwasi uliokuwepo kuhusu ukaribu wa Tanzania na China, kwani hii ni mara ya kwanza kwa Rais wa Tanzania kufanya ziara nchini China tangu aingie madarakani.

Pia mara ya kwanza katika kipindi cha karibu miaka minane tangu rais wa Tanzania afanye ziara nchini China. Ikumbukwe kuwa mtangulizi wa Rais Samia yaani marehemu John Magufuli, pamoja na yeye mwenyewe Samia Suluhu alipokuwa makamu wa Rais, hawakufanya ziara nchini China katika kipindi chote alipokuwa madarakani. Ziara hii imeondoa wasiwasi wowote wa kisiasa uliokuwepo

Kwa upande wa kiuchumi ziara hii imeonekana kuwa na mafanikio makubwa kwani imetangaza fursa nyingi za ushirikiano wa kunufaisha pande mbili. Jumla ya mikataba 15 imesainiwa, ikiwa ni pamoja na mambo ya biashara na uwekezaji.

Ikumbukwe kuwa China ni chanzo kikubwa cha uwekezaji wa moja kwa moja kwa Tanzania (FDI), na sasa kuna jumla ya miradi 1,098 iliyowekezwa na China ikiwa na thamani ya dola za kimarekani bilioni 9.6 na kuzalisha nafasi za ajira laki 1.31. Mikataba hiyo 15 itaenda kuimarisha hadhi hiyo ya China na kuendelea kuinufaisha zaidi Tanzania.

Katika miaka ya hivi karibuni, kupitia mipango mbalimbali ya ushirikiano kati ya China na Afrika, hasa pendekezo la “Ukanda mmoja, Njia moja” (BRI) na Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), nchi mbalimbali za Afrika zimekuwa zikinufaika moja kwa moja kwa miradi ya ujenzi inayofadhiliwa na China.

Safari hii kupitia BRI Rais Samia na Rais Xi wamesaini makubaliano ya mkopo wa ujenzi wa sehemu ya pili (Terminal 2) ya uwanja wa ndege wa Zanzibar wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 56.72.

China pia kama ilivyoahidi mara kwa mara kuwa itaongeza uagizaji wa bidhaa za kilimo kutoka katika nchi za Afrika, imezidi kutekeleza ahadi hii wakati wa ziara ya Rais Samia.

Pande mbili zimesaini makubaliano ya China kuruhusu maparachichi mabichi pamoja na bidhaa za samaki kutoka Tanzania kuingia kwenye soko. Hii ni fursa kubwa kwa wakulima na wavuvi wa Tanzania, na hata kampuni za China zinazopenda kuwekeza kwenye biashara kwenye maeneo hayo.

Balozi wa Tanzania Bw. Mbelwa Kairuki amesema muda mfupi baada ya habari kuhusu makubaliano hayo kutangazwa, kampuni ya Alibaba ya China imetangaza utayari wake wa kuwa jukwaa la kutangaza na kuuza bidhaa hizo.

Lakini mbali na thamani ya kiuchumi ya ziara ya Rais Samia nchini China, ikumbukwe pia ziara hii imefanyika siku chache tu baada ya mkutano mkuu wa chama cha kikomunisti cha China (CPC), na Rais Samia ni mmoja kati ya viongozi wa mwanzo kabisa kukutana na Rais Xi, hii inamaanisha kuwa awamu hii ya uongozi wa CPC imedhamiria kufanya kazi kwa ukaribu na Tanzania.

Na pia ni kipindi ambacho virusi vya COVID-19 bado vinaleta matata, lakini viongozi hao bila kujali hatari hiyo wameweza kukutana na kufanya shughuli za kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zao.