NA ASIA MWALIM
WANAHARAKATI wa Kitaifa na Kimataifa kutoka mashirika na Asasi mbali mbali, kwa muda sasa wameingia kwenye hamasa inaychagiza wanawake nao kushiriki na kushika nafasi muhimu za uongozi kwani hali hilo si wanaume peke yao.

Chagizo za wqanaharaki zinajikita Zaidi kuondoshwa mila, desturi, tamaduni, sera na hata sheria ikilazimika pia kufuata kwa makubaliano na mikataba inayotoa nafasi wanawake kuchukua nafasi za uongozi.

Katika Makala haya yanataka kueleza na kuonesha changamoto zinazowakabili wanawake katika harakati za za kushiriki katika mifumo wa demokrasia, siasa na nafasi mbalimbali za uongozi hapa Zanzibar.

“MIFUMO ndani ya vyama vya siasa Zanzibar bado haijatoa kipaumbele kwa wanawake, hali inayosababisha ushiriki mdogo wa kundi hilo katika uongozi na michakato ya kidemokrasia, kuanzia ngazi za shehia, wilaya majimbo hadi taifa”.

Kauli hiyo aliitoa mmoja kati ya wanawake aliyewahi kugombea nafasi ya uwakilishi katika chama cha CUF mwaka 2015, ambaye hakupenda kubainishwa jina lake katika makala haya.

Makala haya yanataka kuelezea na kuonesha changamoto zinazowakabili wanawake katika harakati za kushiriki katika mfumo wa demokrasia, siasa na nafasi mbali mbali za uongozi.

“Wanawake wanaoteuliwa kuwania nafasi za uongozi ni kidogo sana, fursa hazipo sawa, wanaoshinda ni kidogo sio sawa na wanaume tunataka demokrasia yenye usawa”, alisema.

Kwa mfano mwaka 2020 kati wagombea 32 nafasi ya urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, wanawake watano tu walijitokeza na kati yao hakupita hata mmoja katika nafasi ya wagombea watano waliopitishwa.

Changamoto nyingine ni kutawaliwa na siasa za kupakana matope, kuanzia kwenye chama, familia, wagombea wenza, hadi jamii inayotuzunguka.

Mwanachama huyo alisema changamoto nyingine ni mila na desturi zenye mtazamo potofu zinamchukulia mwanamke kama mtu dhaifu asiyestahiki kuongoza badala yake kukaa nyumbani kutunza familia na mara nyengine mawazo yake kuto thaminiwa, hivyo kuathiri maendeleo ya kina mama.

Pengo jengine linalowaumiza wanawake ni malezi yasiyo mjenga mtoto wa kike kujiamini, na kumpa nafasi kushiriki katika maamuzi ya familia, na kujenga hofu kutokana na vitisho vinavyofanywa na jamii kwa wanawake wanojitokeza kuwania nafasi za uongozi.

Samaki mkunje angali mbichi, huu ni msemo unaothibitisha kuwa wanawake wanapaswa kupewa elimu ya uongozi wakiwa na umri mdogo ili kuwajenga uwezo katika suala la uongozi.

“Uhamasishaji na mafunzo ya uongozi utasaidia wanawake kuwa majasiri na kujitokeza kwa wingi, kuwania nafasi za matawi, wadi, jimbo, mkoa hadi taifa, itakuwa fursa nzuri kwao na jamii kiujumla,” alisema.

Saumu Ali Mahfoudh, kutoka Kidongochekundu alisema, mwaka 2025 anatarajia kugombania nafasi ya udiwani, ingawa alikosa elimu ya uongozi mapema, pia uwezo mdogo wa familia yake kumuwezesha kiuchumi kwani harakati za siasa zinahitaji mipango mapema zaidi.

Ni vigumu wanawake kushughulikia masula ya kuingia katika Uongozi wakati hajajua watoto wake watabaki katika mazingira gani katika masuala ya chakula na usalama wao kutokana na hali ndogo ya kiuchumi.

Nae Halima Ibrahim, mwanamke aliewahi kugombea nafasi ya ubunge katika uchaguzi wa mwaka 2020, alisema changamoto inayowakuta wanawake ni dhana chonganishi zinazoenezwa kuwa eti wanawake hawapendani.

Halima anasema dhana hiyo iko kinyume na uhalisia na kwamba wanawake ni watu wanaoshikamana na kupendana sana, lakini hata hivyo jamii inaaminisha kuwa adui mkubwa wa mwanamke ni mwanamke mwenziwe.

Aidha anafahamisha kuwa ipo mitazamo hasi katika jamii kuwa mwanamke anapoingia katika siasa basi amejishushia heshima na hadhi yake, ambapo kisingizo kikubwa huelezwa hakuumbwa kuwa kiongozi.

“Kuna kasumba nyingi zinazoaminisha kwenye jamii kwamba mwanamke ni mtu asiyefaa kuwa kiongozi, matokeo yake katika uchaguzi wa bunge katika mwaka 2002 tumeshuhudia wabunge walioshinda wanaume ni 257 na wanawake 81, bado tunahitaji kupambana zaidi”, alisema.

Mapengo mengine yaliyotajwa ni vyama vya siasa kuwa na mapendekezo na utaratibu binafsi kwa kumthamini mwanaume zaidi hususan katika majimbo ambayo chama kina matarajio makubwa ya ushindi.

Alibainisha kuwa hali hiyo inakatisha tamaa na miongoni mwa vikwazo ambavyo wanawake wanakumbana navyo wanapowania nafasi za uongozi.

VIONGOZI WA KIKE
Akizungumzia kuhusu ushiriki wa wanawake kwenye uongozi, mwakilishi wa jimbo la Dimani, Mwanaasha Khamis Juma, alisema hali sio mbaya kwa upande wa viongozi wa chama na upande wa serikali katika uteuzi wa wanawake kwenye nafasi mbali mbali.

Mwakilishi huyo alisema nafasi za wanawake barazani zimeongezeka kwenye majimbo kutoka saba hadi nane, kwa mwaka 2015 hadi 2020.

Kwa mwaka 2020, wanaume waliojitokeza kugombea nafasi ya uwakilishi 190 na walioshinda 42, ambapo wanawake walijitokeza kugombea nafasi hiyo hiyo 61 na waliobahatika kushinda ni wanane.

Mwanaasha alisema kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025, wanawake wanapaswa kujiandaa vizuri kushiriki nafasi mbalimbali, kutokata tamaa na wajiamini kwani kwa kufanya hivyo ndiko kutakakowawezesha kuzifikia ndoto zao.

“Dk. Mwinyi kwa kutambua umuhimu wa wanawake na kuwaaamini kwenye uongozi, amewapa nafasi mbali mbali ikiwemo nafasi muhimu kwenye ngazi za maamuzi, hii ni jambo muhimu sana”, alisema Mwanaasha.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar, Tunu Juma Kondo, alisema rushwa ilionekana kutawala uchaguzi wa 2020 ambapo licha ya wanawake wengi kujitokeza, lakini waliopita ni wachache akizungumzia chama chake cha CCM.

Aidha alikiri kutokuwepo sheria ya idadi ya uwiano wa uongozi sawa ndani ya CCM na kwamba kila mtu anapata nafasi kwa kuchaguliwa na wajumbe na sio kulazimisha nafasi maalumu kwa uwiano wa kijinsia.

VITI MAALUMU
Akizungumzia nafasi ya viti maalumu (Nani?) alisema baraza la wawakilishi kupitia vyama vya siasa, nafasi hizo zinagombewa kwa utaratibu na kwa mujibu wa sheria.

Nae Diwani wa wadi ya Chukwani, Fatma Rashid Juma, aliwataka wanawake kuendelea kupigania haki zao za kidemokrasia ili kuwakilisha vizuri katika vyombo vya maamuzi.

Kwa mwaka 2020 wanaume waliojitokeza kugombea nafasi ya udiwani walikua 276 walioshinda 85, ambapo wanawake waliogombania 74 na kushinda 25.

Baadhi ya wanaume walisema ipo haja ya kuzingatia wanawake, kwani wanawake wameelimika na kufahamu mambo mengi wanajifunza kutoka nchi jirani na nchi za kimataifa.

MIKAKATI YA CHAMA CHA MAPINDUZI, KUFIKIA USAWA 50/50
Mmoja kati ya viongozi wa CCM, Khamis Haji Khamis (kiongozi wa ngazi gani), alisema CCM inaunga mkono nafasi ya uongozi kwa mwanamke, pia kama hiyo haitoshi CCM imeweka nafasi maalumu kupitia uongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ili kupata nafasi hizo.

“Sera na katiba, ya CCM imeeleza kwa uwazi na inatekeleza suala la hilo kuzingatia jinsia, kwani akili ni sawa na kuna muda wanafanya maamuzi mazuri kuliko wanaume katika masula ya kujenga nchi na Maendeleo”, alisema.

Alisema CCM inatumia muda mwingi kuhamasisha wanawake kujitokeza ndani ya chama, bunge, uwakilishi na serikali kiujumla, 2005 mwanamke wa kwanza alishika nafasi ya makamu wa Rais, wakati huu amekua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imethibitisha hilo.

Aliwataka wadau wa maendeleo kuendelea kutoa elimu ya uraia ili wanawake wajue haki zao katika jamii, na kuondoa vizingiti vyao kwa kuupinga usemi unaodai hawapendani wenyewe kwa wenyewe.

MTAZAMO WA VYAMA VYA SIASA
Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo, Juma Duni Haji, alisema chama hicho hakina mfumo dume, akitoa mfano kwenye sekretieti ya uongozi ambacho ni chombo kikubwa, imezingatia uwiano sawa wa nafasi 10 wanawake 10 wanaume.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA Zanzibar), katika uchaguzi wa mwaka 2015, idadi ya wanawake walioteuliwa kugombea viti maalumu ni ndogo sana, mfano katika chama cha CCM waliweka asilima tisa, Chadema asilimia sita, CUF asilimia 11, ACT Wazalendo asilimia 15.

NAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII
Kwa upande wake. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Zanzibar, Abeda Rashid alisema, licha ya changamoto zinazowagusa wanawake, lakini wamenufaika na fursa nyingi za uongozi nje ya mifumo vya vyama vya siasa.

Akitoa mfano Abeda alisema kuna nafasi muhimu katika taasisi mbalimbali serikali zinashikiliwa na wanawake ikiwemo kwa mara ya kwanza nafasi aliyokuwa nayo yeye ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, kuongozwa na mwanamke mwanamke mwenye ulemavu.

Alisema pia wapo viongozi walioteuliwa kushuka nafasi muhimu kwa mahitaji ya wanawake akiwemo Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee wanawake na Watoto mwanamke.

“Kwa sisi watu wenye ulemavu tunashukuru sana serikali haijatuacha nyuma, tunampongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuwaona wenye ulemavu na kuwaamini katika nafasi kama hizo hasa ukizingatia hali zao” alisema.

Aliwapongeza wadau maendeleo na taasisi mbali mbali ikiwemo WILDAF, TAMWA, JUWAUZA, kwa kuwa mstari wa mbele kuwashirikisha wanawake kwenye mafunzo ya kuwezesha kushika nafasi za uongozi.

WIZARA HUSIKA
Nae, Katibu Mkuu wizara ya Maendeleo, Jinsia na Watoto Zanzibar, Maryam Abdallah Mabodi, alisema hali ya uongozi Zanzibar iko vizuri, kutokana na idadi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanawake kufikia 29 na wanaume 48.

Kati ya wajumbe wanawake 29, wajumbe wanane ni kutoka katika majimbo na 21 wameingia kupitia viti maalumu na kwamba hadi kufikia mwezi Agosti mwaka 2022, Zanzibar ina mawaziri wanawake 5 kati ya mawaziri 18.

Alibainisha kuwa idadi ya masheha wanawake imeongezeka kutoka 33 kati ya masheha 308 sawa na asilimia 9.7 kwa mwaka 2018 hadi masheha 55 kati ya masheha 332 kwa mwaka 2020, sawa na asilimia 14.

“Azma ya kuongeza ushiriki wa wanawake kufikia 50 kwa 50, inahitaji ushiriki wa wadau mbali mbali kama sera ya jinsia Zanzibar 2026 ilivyo jieleza, ikiwemo kutoa elimu ya ushiriki wa wanawake katika uongozi na utashi”, alisema.
Hata hivyo alisema Wizara hiyo imeandaa mikakati ya kuhamasisha wanawake kugombania nafasi mbali mbali, kwa kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali, kuwaunganisha na fursa za mikopo na masoko ili kujiinua kiuchumi.

Katika hatua nyengine alisema wizara inategemea kutekeleza programu ya masuala ya uongozi, ambayo itatekelezwa na chuo cha diplomasia na uongozi.

“Vikwazo vinavyokwamisha ushiriki wa wanawake katika uongozi ni pamoja na uwezo mdogo wa kifedha za kumuwezesha katika kugombania nafasi za uongozi, mitazamo ya jamii kuwa na imani potofu za kidini kuwa mwanamke hawezi kuwa Kiongozi, ambapo inachangiwa na mfume dume ambao ujenzi wake una historia ndefu katika maendeleo ya mwanadamu” alisema.

KWA MUDA GANI TUTARAJIE MABADILIKO
Akizungumzia suala la mabadiliko, Katibu Maryam alisema kwa kiasi fulani mabadiliko yamepatikana kulingana na takwimu zinavyoonesha, hata hivyo tatizo kubwa linalokwamwisha mabadiliko ni mitazamo ya jamii dhidi ya mwanamke ambalo ni suala gumu kulibadilisha mara moja.

Ili kuongeza idadi ya wanawake kufikia usawa wa 50 kwa 50, ni vyema kushirikiana kuwezesha wanawake kiuchumi, kuwajengea uwezo watoto wa kike, kuhamasisha wanawake kushika nafasi katika vikundi vya ushirika, vikundi vya uzalishaji maji ili kuyoa fursa za kujifunza na kujiamini.

Aliwashauri viongozi wa vyama vya siasa kuweka mikakati maalumu ya kuwawezesha wanawake kugombania na kuwapa nafasi hizo pia kutekeleza programu zinazohusisha wanaume kushiriki kupigania haki za usawa kwa wanawake na wanaume.

KATIBA YA ZANZIBAR
Kwa mfano katiba ya Zanzibar yam waka 1984, katika kifungu 21(2) kila mzanzibari anayo haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomuhusu na yanayohusu taifa lake.

Aidha katiba hiyo katika marekebisho ya 2010 imeeleza wazi kuwa katika kifungu nambari 67 (1) kuwa kutakuwa na wajumbe wa baraza la wawakilishi wanawake kwa idadi ya asilimia 40 wa wajumbe wote wa kuchaguliwa katika majimbo.

SERA TUME YA UCHAGUZI ZANZIBAR (ZEC)
Katika kuhakikisha kuwa wanawake na makundi yaliyo pembezoni haki zao zinazingatiwa katika michakato ya demokrasia na uchaguzi mwaka 2015 ZEC ilitengeneza sera ya jinsia ambayo lengo lake ni kuhakikisha kuwa ushiriki na uwakilishi uliosawa wa raia wote, ingawa sera hii haikuzingatiwa ipasavyo hasa kwa vyama vilivyosimamisha wagombea katika uchaguzi huu mkuu.

DIRA YA 2020
Dira ya Zanzibar lengo nambari 5 imeeleza kuwa kuhusu kuwaendeleza wanawake kwa kuwainua na kutoa nafasi za uongozi kwa wanawake sambamba na kuongeza fursa za kuwa wenza katika vyombo vya utoaji wa maamuzi katika masuala ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na katika ngazi zote za utawala.

DIRA YA ZANZIBAR 2050
Aidha Dira ya Zanzibar katika maazimio ya 2.5.1 hadi 2.5.9 yameeleza Jinsi gani masuala mbali mbali ya usawa wa jinsia na kuondoa unyanyasaji wa kijinsia pamoja na kuimarisha mifumo ya uwezeshaji wanawake ikiwemo kuinua na kutoa nafasi za uongozi kwa wanawake katika jamii.

Pia kuongeza fursa na kuwawezesha katika vyombo vya kutolea maamuzi na kwenye shughuli za uchumi, kijamii, siasa katika ngazi zote za utawala na huduma za sheria.

SERA YA JINSIA YA ZANZIBAR
Aidha katika sera hiyo ya jinsia sura ya 4 katika nambari 4.1 inaeleza ushiriki wa wanawake katika vyombo vya utoaji wa maamuzi katika ngazi zote ni mdogo, Hivyo serikali kwa kushirikiana na wadau wengine watachukua juhudi za makusudi kuona kuwa makundi yote na yaliyopembezoni wanapata fursa hiyo.

ITIFAKI YA SADC
SADC ambayo ni Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika, ambapo mkataba wake wa kikanda uliotiwa saini mwaka 2008 wenye vifungu unaeleza kuondoa utafauti na kuwatenga wanawake katika Nyanja mbalimbali za maendeleo na kuwasaidia katika usawa wa kijinsia nchi wanachama.

Ambapo katika kifungu cha nambari 12 kinasisitiza ushiriki sawa wanawake kufikia asilimia 50/50 kwenye Nyanja za maamuzi, serikalini na taasisi binafsi.

JUKWAA LA UTENDAJI KAZI LA BEIJING
Mpango wa utekelezaji wa Beijing katika maelezo ya dhamira nambari 7 ya mpango huo imeeleza kuhusu uwezeshaji wa wanawake na ushiriki katika vyombo vya maamuzi kwa kuangalia uwiano wa kijinsia kwenye ngazi zote za uongozi.

ITIFAKI YA MAPUTO
Haya ni makubaliano yaliyofanyika tarehe 11, Julai 2003 nchini Msumbiji katika mji wa Maputo, katika kipengele nambari 9 cha makubaliano hayo imeonesha haki ya kushiriki wanawake katika siasa sambamba na kushiriki katika mchakato wa vyombo vya kutoia maamuzi.

MKATABA WA CEDAW
Huu ni mkataba wa CEDAW wa kimataifa ambao unapinga aina zote za udhalilishaji, mkataba huu umeasisiwa mwaka 1979, katika mkataba huu kwenye kifungu chake cha 7 kimeeeleza wazi wanawake kushiriki katika siasa na maisha ya kijamii.

Pia umeeleza kuweko kwa usawa baina ya mwanamke na mwanamme katika uchaguzi na mchakato mzima wa upigaji kura sambamba na nafasi za kushika madaraka, kwa mantiki hiyo basi CEDAW ni mkombozi kwa wanawake katika Nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Kwa mukhtadha huo basi ni wazi kuwa katiba, mikataba ya kimataifa haikuzingatiwa ipasavyo katika kutoa fursa sawa ya uongozi baadhi ya vyama vya siasa Zanzibar vilivyoshiriki kwenye uchaguzi mkuu wa 2020.