NA SAIDA ISSA, DODOMA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameiwezesha bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko kupata mkopo wa shilingi bilioni 150 ili waweze kufanya biashara kwa tija.

Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Mkurugenzi wa CPB, Dk. Anselm Moshi wakati akizungumza na wandishi wa habari juu ya vipaumbele vya taasisi hiyo katika mwaka huu wa fedha.

Alibainisha kuwa fedha hizo zimesaidia kuongeza mzunguko wa biashara kutoka shilingi bilioni 15 kwa mwaka jana hadi kufikia shilingi bilioni 52 mwaka huu.

Alifahamisha kuwa katika kipindi hiki ambacho Rais Samia amekuwa madarakani CPB, imepata mafanikio makubwa ikiwemo kutoa kibali cha kukopa fedha kutoka katika benki ya biashara ya CRDB kama mtaji ili iweze kuendesha shughuli zake kwa uhakika.

“Haya ni mafanikio makubwa na yakujivunia ambapo kupitia fedha tulizonazo tumefanya uwekezaji wa kujenga kiwanda kikubwa cha kukoboa mpunga jijini Mwanza ambapo hadi sasa kinafanya kazi na wakulima wa kanda ya ziwa wamepata soko la uhakika”, alisema.

MIPANGO YA CPB

Dk. Moshi amesema katika kuhakikisha wakulima wanakuwa na masoko ya uhakika CPB imejipanga kuongeza uwezo wa kuhifadhi mazao kutoka tani 122,800 inayohiofadhi sasa hadi kufikia tani 600,000 ifikapo mwaka 2025.

Alisema mkakati mwingine ni kuhakikisha wakulima wanalima kwa tija ili wapate mazao mengi ya matumizi ya nyumbani na kwa ajili ya biashara na sasa tumeanza kuajiri maofisa ugani ili wawasimamie wakulima waweze kutumia mbinu za kisasa katika shughuli zao lengo ni kuongeza uzalishaji

ZAO LA NGANO

Kuhusu zao la ngano Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa CPB, imesaidia wakulima kuzalisha ngano kwa tija kupitia mpango wa kilimo mkataba katika mikoa ya Manyara, Kilimanjaro na Arusha ambapo wanapewa mikataba ya kuzalisha zao hilo.

Alisema CPB imejenga kiwanda cha ngano Arusha ambacho kwa mwaka kinasaga tani 36000.

Alisema lengo la kuanzisha kilimo mkataba katika mikoa hiyo ni kuhakikisha kiwanda kinakuwa na malighafi za kutosha na kufanikisha lengo la nchi la kupunguza uagizaji wa ngano kutoka nje ya nchi ambapo hivi sasa tunaagiza ngano yenye thamani ya shilingi bilioni 530 kila mwaka.

“Tumefanya utafiti na tumeona tuna uwezo wa kuzalisha ngano hapa nchini na kuokoa fedha, mikakati tuliyo nayo ni kuhakikisha ndani ya miaka mitano ijayo suala la kuagiza ngano liwe limeisha kabisa”, alisema.